HOME
‘Viongozi wameshindwa kumuenzi’ Nyerere’
Zanzibar. Baadhi ya wanasiasa
na wananchi mjini Zanzibar, wamesema viongozi wengi wameshindwa kufuata
kwa vitendo yale aliyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere wakati wa uhai wake.
Badala yake, tangu kufariki dunia kwake miaka 15
iliyopita, nchi imeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, ufisadi
na kuporomoka kwa maadili ya uongozi nchini.
Walisema hayo walipokuwa wakizungumza na gazeti
hili kwa nyakati tofauti katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 15 ya
kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na kuitaka Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupambana na
vitendo hivyo.
Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatib alisema
mambo yote yaliyokuwa yakipigwa vita na Mwalimu Nyerere, sasa yamekuwa
yakifanywa na baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali ikiwamo
kujihusisha na rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka bila ya
kuchukuliwa hatua kutokana na kuanguka kwa maadili ya uongozi.
“Hata viongozi wanaotajwa kuwa na nia ya kuwania
urais mwakani, hakuna hata mmoja anayefanana na Mwalimu Nyerere kwa
uadilifu na uwajibikaji, tunahitaji kiongozi kama huyo,” alisema Khatib.
Upande wake, Katibu wa Vijana Mkoa wa Mjini
Magharibi (Bavicha), Francis Gebwa Warema alisema Mwalimu Nyerere
amekuwa akienziwa kwa maneno na siyo vitendo, ndiyo maana vita dhidi ya
rushwa na ufisadi imekuwa ngumu.
Alisema Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia
misingi ya utawala bora ikiwamo sheria zinazopiga vita rushwa na uhujumu
uchumi baada ya viongozi kuamua kuliua Azimio la Arusha wakati ndiyo
ulikuwa msingi wa utawala bora.
Naye aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Simai Mohamed Said alisema Serikali zote mbili zinamuenzi
Mwalimu Nyerere, lakini zinahitaji kuongeza nguvu katika kupambana na
vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na
Taifa.
Naye Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma
wa CUF, Salim Bimani Abdallah alisema: “Inasikitisha mambo aliyokuwa
akiyapinga Mwalimu Nyerere kama ubaguzi na ukabila, sasa yanafanyika
ndani ya vyombo vya kutunga sheria.”
“Misingi ya utawala bora imeshindwa kusimama
kutokana na kuanguka kwa maadili ya uongozi... viongozi wetu wameshindwa
kufuata nyayo zake tangu kufa kwa Azimio la Arusha,” alisema Bimani.
Mjini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo amewataka Watanzania kumuenzi kwa vitendo hayati Baba wa Taifa,
Julius Nyerere ili kurithisha kwa vijana uadilifu wake.
Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere yaliyokwenda sambamba na kutolewa zawadi kwa wanafunzi
wa shule za msingi, Magesa alisema ni muhimu Watanzania kumuenzi Nyerere
kutokana na mchango mkubwa alioutoa.
Chapisha Maoni