HOME
Watanzania waachwe wajadili Katiba
LEO Rais Jakaya Kikwete na Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein watakabidhiwa Katiba
Inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba. Tukio hilo litafanyika
mjini Dodoma kwenye Viwanja vya Jamhuri kuanzia saa 6:00 mchana na
milango ya Uwanja huo itafunguliwa kuanzia saa 12:00 asubuhi.
Serikali mkoani Dodoma imesema
imeimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya siku hiyo huku wananchi
wakitakiwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la
kihistoria nchini.
Tukio hilo litahudhuriwa na marais
wastaafu wa Jamhuri ya Muungano waTanzania na Zanzibar, watendaji wakuu
wa serikali zote mbili, viongozi wengine wakuu wastaafu, maspika
wastaafu, waheshimiwa mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa,
taasisi za kidini, zisizo za kiserikali na wamiliki wakuu wa vyombo vya
habari.
Vilevile kutakuwepo na makundi
mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ni wafugaji,
wakulima, wavuvi, wanawake, vijana, wazee, wachimbaji madini wadogo,
walemavu, wasanii na wengineo.
Tukio hilo la leo linahitimisha safari
nzito iliyokuwa ikiandamana na milima na mabonde kutoka kwa wajumbe wa
bunge hilo maalumu chini ya Mwenyekiti wake, Samuel Sitta huku katiba
hiyo Inayopendekezwa ikibaki mikononi mwa wananchi ili kuweza kuwa
Katiba kamili.
Kutokana na hatua hiyo, napenda kuunga
mkono kauli ya Jukwaa la Katiba iliyotolewa jana na kueleza bayana kuwa
Watanzania wanatakiwa kuachwa huru kujadili katiba hiyo ili muda wa kura
ya maoni utakapofika, waweze kufanya uamuzi sahihi bila kushawishiwa na
vyama vya siasa au makundi mengine yoyote.
Kuendelea kwa vyama vya siasa au makundi
mbalimbali kupiga kampeni na kutoa matamko ambayo yanakidhi matakwa ya
vyama hivyo au makundi mengine, kutafanya Watanzania kupiga kura ya
maoni kwa shinikizo la vyama vya siasa au madhehebu ya dini.
Ni dhahiri kuwa tukio la leo la
kumkabidhi Rais Katiba Inayopendekezwa litafungua mlango kwa wananchi
kusoma na kujadili katiba hiyo Inayopendekezwa na kupata majibu
yatakayowawezesha kupiga kura mara muda utakapofika.
Nasema hivyo kutokana na ukweli kuwa
kuendelea kwa wanasiasa na makundi mbalimbali kutoa mapendekezo yao na
maoni katika mijadala na vyombo vya habari ni kuwachanganya wananchi na
kuwashawishi kupiga kura kwa maslahi yao.
Kuendelea kwa makundi mbalimbali kutaka
wananchi wafuate matakwa yao ni kuwanyima uhuru na kufanya nia nzuri ya
Rais Kikwete kupatikana Katiba mpya isiwe na maana.
Naona kwa wakati huu, ni muda muafaka wa
wananchi kusoma Katiba Inayopendekezwa na kuielewa huku vyombo vya
habari vikitoa elimu kwa baadhi ya vipengele vya katiba hiyo ili
wananchi waweze kufanya maamuzi.
Kwa wakati huu ni vyema kusahau
changamoto zilizojitokeza katika Bunge Maalumu lililomalizika, bali
kuelekeza macho yetu kwenye kujadili na kuelewa yaliyomo katika katiba
hiyo kwa nia ya kuhakikisha haki inapatikana katika suala hilo.
Kutokana na suala hilo, ni vyema
wananchi kutokubali kutekwa na wanasiasa au kundi lolote kwa kufanya
yale wanayotaka kwani itakuwa ni sawa na kukana haki yao ya kupiga kura
kwa lile wanaloona linafaa kwa nchi na kwa manufaa yao na badala yake,
watakuwa wanafanya maamuzi kwa maslahi ya wengine.
Ni wakati muafaka wa kuhakikisha
wanasiasa na makundi mengine katika jamii yanakubali kuwaachia wananchi
wapate nafasi yao sasa ya kufanya maamuzi sahihi kwani kuendelea
kuwachanganya hakuwatendei haki.
Kwa wakati huu wa kujadili katiba hiyo
Inayopendekezwa uhuru na uvumilivu unahitajika miongoni mwa wananchi ili
kuweza kufikia muafaka kwa baadhi ya vipengele ambavyo wananchi
wanakinzana navyo.
Chapisha Maoni