HOME
UKAWA WATAKA KICHWA CHA WAZIRI ALIYEWEKWA KIPORO "RAIS HALIAMINI BUNGE"
Profesa Muhongo |
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umelitaka Bunge
kuiwajibisha Serikali ikiwa Rais Jakaya Kikwete atashindwa kutekeleza
maazimio ya Bunge ikiwamo kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Wakizungumza jijini Dar es salaam jana, viongozi hao walisema
endapo Rais atashindwa kumwajibisha Profesa Muhongo, basi wabunge wao
watawasilisha hoja na kushawishi wengine kupiga kura ya kutokuwa na
imani na waziri mkuu na umoja huo utaitisha maandamano nchi nzima.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim
Lipumba alihoji kwa nini Rais Kikwete anasita kumwondoa Profesa Muhongo
wakati Bunge lilishatoa maazimio.
Alisema Bunge linalowakilisha wananchi zaidi ya
milioni 45 liliazimia uteuzi huo utenguliwe lakini akaelezea kushangazwa
kwake na hatua ya Rais kusema bado anachunguza.
“Hivi Rais anachunguza nini, haliamini bunge? Kama
anavyoteua mawaziri pia ana madaraka ya kutengua nafasi zao, sasa
anasita nini wakati azimio la Bunge limemwelekeza. Kama Rais Kikwete
atashindwa kumwajibisha Muhongo atakuwa ameshindwa kutekeleza moja ya
maazimio ya Bunge na Ukawa utaliomba Bunge kuiwajibisha Serikali.”
Alisema hotuba aliyoitoa Jumatatu wakati
akiwahutubia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, haijakidhi matarajio ya
wengi kwani kuna maazimio hayajatekelezwa.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF,
alisema Rais amekataa kutekeleza azimio la kutaka mitambo ya IPTL
itaifishwe na kutoa sababu ambazo hazina mashiko.
“Tangu mitambo ya IPTL imefungwa Taifa limepata
hasara kubwa kwa sababu umeme unaouzwa ni wa gharama kubwa kuliko
mitambo yoyote ya umeme inayotumika katika bara la Afrika, Taifa
limeingia hasara kubwa, Rais aitaifishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema katika hotuba hiyo Rais Kikwete alionyesha
kuipendelea IPTL na kuikandamiza Tanesco wakati akielezea kuwa fedha za
escrow zilikuwa mali ya IPTL.
Alitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya
wote waliohusika na ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na wengine
walionufaika nazo.
“Sheria ya maadili itungwe upya ili iweke uwazi wa mtu yeyote kuona taarifa ya mali za viongozi.”
Ads by SavePass 1.1Ad Options
Mbatia na Dk Slaa
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliwataka viongozi wa
dini kuliombea Taifa katika kipindi hiki ambacho mihimili ya dola
inapingana.
“Tuna matatizo makubwa, malori ya fedha yanachotwa
benki kwa siku moja lakini Usalama wa Taifa hawashtuki, viongozi wa
dini liombeeni Taifa, tuna mtikisiko,” alisema Mbatia.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema
amesikitishwa na hotuba ya Rais kwa kutowataja wahusika waliochota Sh73
bilioni katika Benki ya Stanbic wakati kuna Idara ya Usalama wa Taifa.
“Hivi kweli Serikali yenye Usalama wa Taifa haiwafahamu waliochota fedha hizo?” alihoji Dk Slaa.
LHRC yashangazwa
Wakati viongozi hao wakisema hayo, Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kusikitishwa kwake na
utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge juu ya sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo -
Bisimba alisema katika taarifa yake kuwa hotuba ya Rais Kikwete kupitia
kwa wazee wa Dar es Salaam
Jumatatu iliyopita, iliikumbatia kampuni ya IPTL na kutupa maazimio
mengi ya Bunge kutokana na kutochukuliwa hatua zilizotarajiwa.
Licha ya kwamba tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick
Werema ameshajiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, kufutwa kazi na Katibu Mkuu wa Nishati na
Madini, Eliakimu Maswi kusimamishwa kazi, Dk Bisimba alisema Rais
hakuchukulia suala hilo kwa uzito na kwa kiwango kinachotakiwa.
Alisema badala yake, hotuba ya Rais ilijaa
masihara katika kashfa nzito inayoipa kibarua kigumu Serikali katika
kupambana na rushwa.
Alimtaka Rais Kikwete apokee heshima aliyopewa na
Bunge ya kufanya uamuzi na kwamba kutofanya hivyo kutamshushia heshima
kwa Watanzania.
Dk Bisimba alisema masuala ya escrow, umiliki wa
PAP/IPTL, tuhuma za rushwa na kodi za Serikali yalikuwa
yameshafafanuliwa na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) lakini kwa bahati mbaya, Rais aliyarudia upya na kuegemea upande wa IPTL.
“Rais katika hotuba yake alikuwa anapangua kila
hoja kiasi kwamba alitoa hitimisho la kuwa fedha zilizokuwa kwenye
akaunti ile hazikuwa za Serikali, bali za IPTL, jambo ambalo si sahihi.”
Alisema kauli ya kutaka uchunguzi uendelee juu ya masuala hayo
inaibua utata wa uchunguzi ufanywe na nani tena zaidi ya Bunge kupitia
CAG na Takukuru na kwamba matokeo yake apewe nani?
Mdee: Tibaijuka abanwe zaidi
Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Halima Mdee alisema Rais Kikwete anatakiwa kumchukulia hatua
zaidi Profesa Tibaijuka ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma.
Kauli hiyo ya Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe
(Chadema) inatokana tuhuma za ukosefu wa maadili kwa waziri huyo baada
ya akaunti yake binafsi kuingiziwa Sh1.6 bilioni katika kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo alisema zilikuwa za kusaidia shule.
Mdee alisema: “Suala hili halitakiwi kuishia kwa kumvua uwaziri.
Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu anatakiwa kuchukua hatua zaidi ya hapo ili kuwa fundisho wa watumishi wengine.
“Rais Kikwete ndiye anayeweza kuifanya nchi hii
ikaendelea zaidi na yeye mwenyewe anaweza kuwafanya viongozi wake wakawa
wawajibikaji na waadilifu lakini ukisema mtu anakosea unamfukuza kazi,
tutakuwa tunafanya mambo ya kuigiza. Rais azingatie ipasavyo maazimio ya
Bunge kama yanavyosema.”
Alipoulizwa atamkumbuka kwa lipi waziri Profesa
Tibaijuka katika wizara hiyo, Mdee alisema, “Katika kipindi chote akiwa
waziri wa ardhi sina cha kumkumbuka kwani migogoro ya ardhi ndiyo kwanza
imeongezeka, wakulima na wafugaji kila kukicha ni mapigano, tunahitaji
mtu atakayeiongoza wizara hiyo ipasavyo na kupunguza migogoro ya ardhi
inayogharimu uhai wa wananchi.”
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Nuzulack Dausen na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Chapisha Maoni