Waamuzi watatu wa soka kutoka Uganda, ndio wakaochezesha mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars ya Kenya utakaofanyika Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi, Kenya.
Waamuzi hao watakaochezesha mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Azam Tv kwa kushirikishi na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) ni Brian Nsubuga atakayepuliza kipenga na wasaidizi wake ni Bugembe Hussein upande wa kulia (line 1) na Katenya Ronald kwa upande wa kushoto (line 2).
Kamishna wa mchezo atakuwa Amir Hassan kutoka Somalia ambako Meneja wa Uwanja wa Moi Kasarani, Lilian Nzile amesema kwamba mazingira uwanja ni mazuri na mipango yote ya mchezo huo imekaa vema ikiwa ni pamoja na usalama uliothibitishwa pia na Kanali wa Jeshi la Polisi, Muchemi Kiruhi OCS wa Kasarani.
Kwa upande wa Kocha Mkuu Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), Charles Boniface Mkwasa atawakosa washambuliaji wake watatu katika kikosi ambacho kitaivaa Harambee Stars.
Washambuliaji hao ni Mbwana Samatta kutoka Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na John Bocco ambaye ni majeruhi wa mguu aliumia wakati wa fainali za Kombe la FA kati ya Yanga na Azam Jumatano wiki hii.
“Madaktari wamempa Bocco saa 72 za mapumziko. Bila shaka kabla ya kucheza na Misri atakuwa amepona,” alisema Mkwasa leo Mei 28, 2016 asubuhi na kuongeza kuwa Samatta ametuma taarifa kukosa mchezo dhidi ya Kenya kwa kuwa ana ratiba ya kucheza mchezo muhimu Mei 30, mwaka huu na matarajio ni kujiunga na timu Juni 1, 2016 kabla ya kuivaa Misri Juni 4, mwaka huu.
Kwa upande wa Ulimwengu, uongozi wa TP Mazembe nao waliomba kumtumia Ulimwengu katika mchezo wa ushindani wa mpinzani wake AS Vita. TP Mazembe na AS Vita ni timu pinzani huko DRC Congo na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukaridhia na Mkwasa sasa amejipanga kukiandaa kikosi bila nyota hao mahiri.
“Katika mchezo huu sitakuwa na professionals (wachezaji wa kulipwa),” alisema Mkwasa ambaye jioni ya leo ameahidi kutoa kikosi cha nyota 11 watakaonza dhidi ya Kenya kesho.
Kwa sasa anaangalia namna ya kuipanga vema safu yake ya ulinzi baada ya kumkosa Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kuonywa mara mbili kwa kadi ya njano hivyo kutojumuishwa kwenye mipango mchezo dhidi ya Misri. Mabeki anaotarajiwa kuanza nao ni Juma Abdul upande wa kulia na Mohammed Hussein upande wa kushoto.
Walinzi wakaoachukua nafasi ya Yondani na Nadir Haroub Cannavaro ambaye hakuongozana na timu katika safari ya Kenya ni Erasto Nyoni, Aggrey Morris na David Mwantika huku viungo wa kati wanaotarajiwa kupangwa ni Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na pembeni ni Farid Mussa na Shiza Kichuya. Washambuliaji watakaotikisa Kenya katika mchezo wa kesho ni Elisu Maguli na Ibrahim Ajib.
“Kipa anaweza kuanza Dida (Deo Munishi) au Aishi Manula. Lakini hao niliokutajia ni proposed team (kikosi tarajiwa), lakini hasa nani anaaza kesho nitakutajia jioni ya leo mara baada ya mazoezi pale Moi Kasarani,” alisema Mkwasa aliyeonekana kujiamini na mipango yake kama lilivyo jina lake la umaarufu la Master.
“Nimeiandaa timu kucheza mifumo miwili ambayo ni 4-3-3 ambao ni mfumo wa kushambuliaji na pale tutakapokuwa tuna-defense (tunazuia) basi mfumo utakuwa ni 4-5-1,” alisema Mkwasa.
Katika mchezo wa kesho Mkwasa anayesaidia na Hemed Morocco na Manyika Peter anayewanoa makipa atapata nafasi ya kubadili wachezaji hadi sita ambao ni utaratibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mechi za kirafiki za kimataifa kadhalika makubaliano katika mkutano wa kabla ya mchezo wa kesho.
Stars iliwasili Nairobi, Kenya jana asubuhi na kupokewa na wenyeji Shirikisho la Soka Kenya iliyowapeleka hoteli ya Nairobi Safari Club iliyoko mtaa wa Koinange, katikati ya jiji la Nairobi ambako mchana kabla ya kwenda mazoezi ilitembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Haule aliyewahakikishia usalama timu hiyo licha ya kuwako kwa taarifa za kuvamiwa.
“Msaada wowote mnaotaka na chochote mnachohitaji tunaomba mtutaarifu tujue namna ya kuwasaidia. Msiwe na wasiwasi kabisa. Hata kama hamjaipenda hoteli, semeni,” alisema Dk. Haule ambaye aliitakia timu mafanikio mazuri katika mchezo wa dhidi ya Harambee na ule wa Mafarao wa Misri.
Viongozi wa msafara wa Taifa Stars, Ahmed Mgoyi na Omar Walii walimweleza Balozi DK. Haule kuridhika na kambi na kwamba hawakupata tatizo lolote hali ilivyo hadi sasa.
Chapisha Maoni