Alisema chama hicho kinatakiwa kujihadhari na watu
wa aina hiyo kwa sababu Uchaguzi Mkuu ujao ni muhimu kuliko chaguzi
zote za miaka ya nyuma kwa sababu ni uchaguzi ambao utaamua mwelekeo wa
Tanzania.
“Tanzania ipo njiapanda. Nasema hivi kwa sababu mambo yote ya
kuiwezesha nchi kufanya vizuri yapo, uchumi unakua vizuri, gesi inakuja,
amani kidogo na utulivu upo, ina vijana wengi wenye hamasa, kilimo
tunaweza kukipanua, ufugaji kuuboresha,” alisema.
Aliongeza, “Kuna njia nyingine ya kuchukua baada
ya kuwapo kwa nyufa nyingi. Kuna tatizo la ajira, lipo suala la Muungano
pamoja na rushwa ndiyo maana nasema uchaguzi ujao ni muhimu. Uchaguzi
huo ndiyo hatima ya Tanzania tuipendayo.”
Akizungumzia sifa za rais ajaye Makamba alianza
kwa kueleza nia yake ya kutaka nafasi hiyo na kusisitiza kuwa sifa anazo
na hatanii katika hilo kama ambavyo watu wengi wanavyodhani kuwa ana
malengo ya baadaye na si sasa.
Alisema kila kizazi cha uongozi wa Tanzania kina
changamoto zake na kusisitiza kuwa hivi sasa Tanzania inatakiwa kuwa na
kiongozi anayetoka katika kizazi kinachotizama mambo ya mbele, si
yaliyopita.
“Kama watu wamefarakana na kugombea uongozi huko
nyuma siyo sababu ya kutafuta uongozi ili kulipiza kisasi na kuendeleza
mafarakano yao.
Kuna dhana kwamba uongozi ni kupokezana kijiti
kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine, sasa ni wakati wa kupokezana
kijiti kutoka kwao kuja kwetu,” alisema.
Alisema rais anatakiwa kuwa mtu asiye na doa la
rushwa, awe na uelewa mpana kuhusu mazingira ya nchi yetu yaliyopo sasa,
changamoto za watu kwa kawaida na uelewa mpana kuhusu dunia ilivyo,
kwani Rais ajaye atajihusisha na ulimwengu, huku akimtolea mfano Rais
Jakaya Kikwete.
“Awe na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania kwa
sababu kama mnavyoona chembechembe za mgawanyiko zimeanza, mgawanyiko
kati ya Tanzania bara na Tanzania Visiwani, mgawanyiko wa kidini na
kikanda,” alisema na kuongeza;
“Awe kiongozi mtendaji, kwa sababu sisi tunazo
sheria, mifumo na mipango, lakini shida ni utekelezaji na kwa kiongozi
tunayemtaka ni yule ambaye hatakuwa mbali na mifumo ya utekelezaji. Si
kiongozi anayetoa hotuba na maelezo mazuri tu, bali kuhakikisha kiongozi
ambaye atatoa adhabu kwa wale ambao watashindwa kutekeleza yale ambayo
tumekubaliana,” alisema.
Alisema taifa halihitaji kiongozi ambaye amewahi
kukaa Serikali kwa miaka 30 hadi 45, kusisitiza kuwa zama hizi
zinahitaji rais mwenye sifa nyingine za ziada.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, bado CCM ni chama
sahihi kinachotakiwa kutoa rais katika uchaguzi ujao kutokana na
historia ya chama hicho pamoja na viongozi na makada wake.
“Nchi ina changamoto nyingi lakini mambo
yaliyofanywa na CCM yanaonekana. Chama kina historia ya uongozi barani
Afrika na misimamo ambayo chama kimeuchukua katika ukombozi wa mtu
mweusi ni historia ya kujivunia sana,” alisema.
Alisema chama hicho kina watu wa aina mbalimbali na kina uwezo
wa kutoa viongozi wazuri, “CCM kinasimamia sera sahihi, nzuri na bora
kwa maendeleo ya mtu. Ukitaja kila kitu, mfano katika kilimo tuna
msimamo na sera na mipango kwenye afya. Hivyo hivyo katika kilimo, afya,
elimu na maji.”
Akizungumzia elimu alisema, “Mfumo wetu wa elimu
lazima tuufumue upya ili tumweke mwalimu na mwanafunzi katikati ya
mazingira mazuri ya mipango yetu ya elimu.”
Alisema bila ya mwalimu aliyeridhika nchi haiwezi
kupiga hatua, kusisitiza kuwa walimu waliopo lazima walipwe vizuri,
kuondoa dhana kwamba ualimu ndiyo fani ya kukimbilia watu wanapokosa
pahara pa kwenda.
“Kuanzisha ukaguzi, malipo, mitalaa, katika mambo
ya kuongoza taifa hili hakuna ambacho sijafikiria katika kulifanya.
Lazima tuamue lugha yetu ya kufundishia iwe ipi kwani mwaka 2007
ulifanyika utafiti na kubaini mwanafunzi wa sekondari walishindwa kusoma
na kutafsri aya ndogo tu ya Kiingereza ya shule ya msingi na mimi
naamini kwamba tunaweza kuziweka lugha zote zikatumika,” alisema.
Alisema mwalimu mwenye motisha anaweza kusaidia kuboresha elimu na mabadiliko ya mitalaa kutokana na uongozi.
Ajira
Akizungumzia tatizo la ajira nchini, Makamba
alitaja mipango madhubuti ambayo kama ikifanyika itamaliza kabisa tatizo
la ajira nchini.
“Hivi sasa kuna vijana 900,000 wa kati ya miaka 15
na 24 wanaingia katika soko la ajira kila mwaka. Watu waliopo katika
soko la ajira ni karibia milioni 22 na idadi hiyo itaongezeka mara mbili
katika miaka 15 ijayo. Mwaka 2030 tutakuwa na watu milioni 45 katika
soko la ajira na hao ni watu wengi mno,” alisema.
Alisema jambo la kwanza ni kurekebisha mfumo wa
elimu ambao utawawezesha vijana kuwa na uwezo na maarifa ya kupata ajira
zinazoendana na uchumi wa kisasa, kutokana na sasa nchi kuwa na vijana
wengi wasiokuwa na maarifa ambao wameishia darasa la saba au kidato cha
nne.
“Tunaweza tukatenga Sh3 trilioni au Sh4 trilioni
kwa ajili ya uwekezaji. Hizi fedha tunaweza kuzipata. Tuanze kwa kufufua
viwanda 11 vya nguo vilivyokufa. Tanzania tunalima sana pamba lakini
pamba inayotumika katika viwanda vya Tanzania ni asilimia 30 tu,
asilimia nyingine yote inauzwa nje,” alisema.
Alifafanua kuwa kama nchi ikiweza kutumia asilimia
70 ya pamba inayozalishwa katika viwanda vya ndani itakuwa imetoa ajira
kubwa.
Alisema ajira pia inaweza kuongezwa katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi nchini kwa kuongeza thamani ya mazao.
“Kuongeza thamani siyo kitu kikubwa, mfano kukamua juisi ni
kuongeza thamani, kutengeneza maboksi na kupaki vizuri matunda ni
kuongeza thamani na kukoboa mahindi na kutengeneza unga wa sembe ni
kuongeza thamani,” alisema.
Pia, alitolea mfano jambo jingine na kupunguza
tatizo la ajira kuwa ni kuweka mikakati ili Mifuko ya Hifadhi za Jamii,
kuanzisha mifuko mikubwa ya kutoa mikopo na dhamana kwa wajasiriamali.
“Jambo jingine, ununuzi unaofanywa na Serikali.
Kila siku serikali inanunua karatasi, vipuri, mafuta, tiketi za ndege,
chakula, maji ya kunywa na mengine mengi. Unaweza kuweka utaratibu
kwamba asilimia 30 ya ununuzi wa serikali uende kwenye kampuni
ndogondogo za vijana na akina mama ili kuwajengea uwezo,” alisema.
Alisema katika miji yote na vijijini, chimbuko
lake la uchumi ni biashara ndogondogo, lakini hakuna taasisi au mamlaka
mahsusi inayojihusisha na kusaidia biashara ndogondogo.
Alisema, “Jambo jingine ni vyuo vya ufundi. Huko
nyuma tuliahidi kwamba kila wilaya itakuwa na chuo cha ufundi na
tunafahamu kuwa mfumo wetu wa elimu vijana wengi wanamaliza darasa la
saba na kidato cha nne, hawaendelei na elimu ya juu. Elimu wanayoipata
haiwasaidii kufanya shughuli yoyote au kupata kazi.”
Aliongeza, “Watu hawa wote wanatakiwa kuchukuliwa
na vyuo vya ufundi ili kujifunza stadi za maisha kama ufundi selemala au
ufundi ujenzi. Utaratibu ni kwamba utakapomaliza chuo katika wilaya
zetu, kama wewe ni fundi selemala unaondoka na vocha ya kukuwezesha
kupata vifaa ili kuanza biashara ya ufundi uliousomea.”
Alitolea mfano nchi Ujerumani kuwa wana mfumo
mzuri wa elimu, kufafanua kuwa magari wanayotengeneza ya nchini humo
aina ya Mercedes Benz, asilimia 70 ya vifaa vinavyotengeneza magari
hayo, vimetengenezwa na kampuni ndogo za watu ambao hawakufika vyuo
vikuu.
“Hata kwetu tuna vyuo vya ufundi 150, sasa kama
vikiwa vinatoa watu wenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi za mikono na
kuzalisha mali faida yake kwa soko la ajira na uchumi itakuwa kubwa
sana,” alisema.
Alisema, “Siku hizi kuna misamaha ya kodi ambayo
mtu hupewa kwa kuja tu nchini. Misamaha ya kodi inatakiwa kubadilishwa
na kuwekewa kigezo kingine. Kama wewe ukiweza kuajiri watu 1,000 kwa
kadri utakavyoongeza watu 1,000 katika biashara yako unapata mwaka mmoja
wa msamaha wa kodi, ukiongeza 2,000 utapata msamaha kwa miaka miwili.”
Ataja mali zake
Akitaja mali zake Makamba alisema, “Katika vitu
ambavyo havinisumbui kabisa ni suala la kumiliki mali, huwa ninapata
lawama kubwa kwa ndugu na jamaa kwamba nina nafasi, lakini sina miradi
mikubwa wala biashara. Mimi sivyo nilivyo, mimi maisha ya kuishi kwa
mshahara na posho.”
Alisisitiza, “Kijijini nina kashamba kadogo, nina
gari ambalo anatumia mke wangu na tuna nyumba ambayo tulipewa zawadi
wakati wa harusi yetu. Sina biashara yoyote ambayo ninaendesha na
sijawahi kufikiria kujilimbikizia mali na hii haijalishi kama nipo au
sipo katika uongozi.”