HOME
Keissy alianzisha tena bungeni
Keissy alianzisha tena bungeni
Kessy alisimama bungeni hapo saa 5:52 asubuhi
kutoa mchango wake kuhusu Katiba akijikita zaidi katika suala la muundo
wa Muungano na kusema kwamba Zanzibar inabebwa na Tanganyika.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika inabeba mzigo
mkubwa ambao haubebeki, hapa tunahudumia wabunge 83 kutoka Zanzibar
ambao wanatibiwa wao na wake zao na watoto kwa gharama za Tanganyika
wakati hawachangii,” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani kwa Tanganyika
kubeba mzigo mkubwa kama huo wakati katika Jimbo lake la Nkasi wananchi
wanalia na shida ya maji.
Alisema katika Kamati yao Namba Moja, Gavana wa
Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alitoa semina iliyoonyesha kuwa Zanzibar
haichangii chochote kwenye Muungano na kuwa hata mishahara wakati
mwingine wanategemea Tanganyika.
Keissy alisema wananchi wakilijua jambo hilo,
wataikataa Katiba inayopendekezwa na kuitupilia mbali kwa kuwa inatoa
upendeleo kwa Wazanzibari na kuikandamiza Tanganyika.
“Mimi naweza kuwa na wanawake sita, nikazaa nao
lakini kila mtoto anaendelea kutunzwa na baba yangu, jambo kama hili
halivumiliki hata kidogo japo najua kuwa ukweli unawauma,” alisema huku
baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wengine kumpinga na wengine kuomba
mwongozo wa mwenyekiti.
Alipinga suala la rais wa Zanzibar kuwa makamu wa
rais wa Muungano kwa maelezo kuwa katika mfumo wa vyama vingi jambo kama
hilo haliwezekani na kuhoji itakuwaje awe makamu wa kwanza wa rais
wakati hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara?
Baada ya kauli hiyo, kelele za wajumbe kutoka
Zanzibar ziliongezeka baadhi wakisimama na kuwasha vipaza sauti
kumshambulia Keissy, “chizi huyo, chizi huyo, hafai kwanza ni Mwarabu,”
zilisikika sauti huku nyingine zikimtaka aombe radhi.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alimpa nafasi
mmoja wa wajumbe hao, Fatuma Hamis Salehe kutoa taarifa, ndipo alisema
wajumbe wa Zanzibar wapo kisheria ndani ya Bunge hilo na wala si kwa
fadhila, hivyo akamtaka Keissy kuomba radhi.
Hata hivyo, Kessy alijibu akisema, “Siko tayari
kuomba radhi katika jambo hili, mimi nazungumzia masuala ya Ndullu,
alikuja pale katika kamati na kwamba tangu kifo cha Karume hamjawahi
kuchangia, mnaposema mimi Mpemba au Mwarabu basi ninyi ni Wakongo,”
alisema kwa sauti ya juu.
Alisema posho wanazolipwa bungeni hapo, zimetoka upande wa Tanganyika na Zanzibar haijachangia hata senti moja.
Baada ya hapo kelele ziliongezeka sawia na idadi
ya waomba mwongozo, Mjumbe kutoka Kundi la 201, Ally Juma Khatibu,
alisimama hata bila ya kupewa ruksa na kuanza kuzungumza kwa ukali
akisema Kessy ni mbaguzi na mtu anayestahili adhabu kali.
Baadaye alipewa nafasi Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye
aliwataka wajumbe kuwa wavumilivu na kupuuza baadhi ya mambo kwani
kipindi kilichobakia ni cha kumalizia.
Alifuata Mjumbe, Mahmoud Thabit Kombo aliyesema
Keissy hajui historia kwani Zanzibar ilipoteza utambulisho wake katika
kiti cha Umoja wa Mataifa na kuiachia Tanzania, jambo ambalo nchi hiyo
ndogo inastahili kupongezwa.
Mjumbe mwingine, Abdalla Sharia Ameir alimtuhumu
Keissy kuwa ni mtu mwenye asili ya Arabuni ndiyo maana anapiga kelele
kwa Waafrika na kutaka akapimwe akili.
Ameir alimtaka Keissy atoke nje kama ni mwanamume
na hapo alianza kutangulia lakini alipoona hakuna wa kumfuata, alirudi
hadi karibu na kiti alichokaa Keissy ndipo wajumbe wengine walipoingilia
kuwatuliza.
Kwa upande wake, Hamad Rashid Mohamed alimwita Keissy mchochezi asiyejua historia ya Tanganyika na Zanzibar katika Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu,
Stephen Wassira alimtahadharisha Keissy kuwa mchango wake unaweza kuzua
vita na kumtaka awe makini wakati wote na ndimi zake... “Japo ni maoni
yake, lakini mengine yana gharama kubwa, lazima uchunge ulimi wako.”
Baadaye, Sitta alisimama akimtaka Keissy aombe
radhi, jambo alilolikubali kiaina akisema, “Nilichokizungumza kina
ukweli katika Bunge la Muungano lakini kama nimekosea naomba msamaha,”
alisema.
Asindikizwa kutoka
Baada ya Sitta kuahirisha kikao, Keissy alifuatwa
na mmoja wa wahudumu wa Bunge, Waziri Kizingiti na kumshika mkono hadi
kwa wapambe wa Bunge waliomchukua na kumpeleka katika Ofisi ya Spika
iliyopo kwenye jengo la Bunge na baadaye kutoka naye nje wakitumia
mlango unaotumiwa na Waziri Mkuu kuingia na kutoka bungeni akiwa
amezungukwa na askari wa Bunge watano hadi mlango wa kutoka nje ya eneo
la Bunge ambao kwa kawaida hutumiwa na viongozi wakuu wa Serikali na
Bunge.
“Mheshimiwa Keissy? Gari lako liko wapi uende
ukapakie,” alisikika mmoja wa wapambe akimuuliza Keissy ambaye alisema
hana gari akiwataka wamwache arudi ndani akachukue begi lake lakini
alikataliwa na badala yake alipelekwa hadi sehemu ya ukaguzi katika
lango la kuingilia na kupewa kiti huku akiwa amezungukwa na wapambe hao.
Nje ya Ukumbi wa Bunge, wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wakimsubiri atoke kwa takriban dakika 30 bila mafanikio.
“Keissy yuko wapi? Kama mwanamume kweli atoke,
wanamfichaficha ndani ili iweje? Tumechoka na matusi yake,” alisikika
mmoja wa wajumbe akisema.
Akizungumza baada ya kufika hotelini, Keissy alisema hakuna
anachoogopa kwa sababu alisimama katika ukweli katika mazungumzo yake.
“Mimi nilizungumza badala ya Watanganyika na ukweli ndiyo huo hata kama kuna watu ambao hawataki kuusikia,” alisema Keissy.
Alisema aliyasema maneno hayo kwa nia ya kutaka
kuboresha Muungano katika Katiba inayoandikwa hivi sasa na si kuuvunja
kama alivyotafsiriwa na Wassira.
Chapisha Maoni