HOME
Mbowe kutinga polisi na mawakili
Mawakili hao wataongozwa na Makamu Mwenyekiti
wake, Profesa Abdallah Safari, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu,
Halima Mdee, Mabere Marando na Peter Kibatala, huku makada wa chama
hicho wakialikwa kuandamana naye kumsindikiza.
Mbowe alitoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa
chama hicho Septemba 14, mwaka huu, akisema maandamano hayo yatafanyika
katika siku ambayo itapangwa katika mikoa yote.
Siku moja baadaye, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo
wa Polisi, Kamishna Paulo Chagonja alimkemea akisema iwapo atafanya
hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa. Pia, Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai (DCI) alimwandikia barua akimwita kuhojiwa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
jana kwamba uamuzi huo ni moja ya maazimio matatu ya kikao cha kwanza
cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi.
“Mbowe ameitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi
kesho (leo). Polisi wameandika barua ya wito huo lakini hawajasema kosa
lake ni nini. Itakuwa saa tano asubuhi na atakwenda na mawakili wote wa
chama,” alisema Dk Slaa mbele ya viongozi wote wa sekretarieti mpya ya
chama hicho.
Akizungumzia wito huo jana, DCI Mngulu alisema
ingawa leo atakuwa Songea, ofisi yake ina watumishi wengi na kwamba
ameshawasiliana naye kwa ujumbe kumfahamisha hilo.
Katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
(Bara), John Mnyika alisema, “Tunawaomba wanachama wa Chadema kujitokeza
Makao Makuu ya Polisi ili kumsindikiza mwenyekiti atakayekuwa
akihojiwa.”
Kwa upande wake, Lissu alisema katika barua ya
wito, polisi wametaja vifungu vya sheria, lakini hawakueleza kosa la
Mbowe ni nini, jambo ambalo linaonyesha jinsi wanavyofanya kazi nyuma ya
kivuli cha chama tawala, CCM.
Akizungumzia madai hayo, Mngulu alisema Kifungu
cha 10 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinajieleza wazi. Kifungu hicho
kinazungumzia kudhamiria kutenda kosa.
Maandamano
Akizungumzia maandamano hayo, Dk Slaa alisema
tarehe rasmi itatajwa baada ya viongozi wa Ukawa kukutana... “Maandamano
yatafanyika nchi nzima, tayari taratibu zimeanza kufanywa mikoani.
Tutaeleza tarehe hiyo. Tumepinga kwa maneno tukitaka Bunge lisitishwe
lakini wenzetu wameweka pamba masikioni. Sasa tunaonyesha chuki na
hasira, polisi watambue kuwa wao wapo 35,000 na wananchi wapo milioni
45.
“Tumenyimwa vibali katika mikutano yetu iliyopita sasa safari
hii wakikataa kutupa kibali tutaandamana tu. Azimio la Kamati Kuu
haliwezi kuvunjwa na Chagonja kwa sababu maandamano ni haki yetu na
tumeshafanya maandamano 100 ya amani nchini.”
Ukawa
Kuhusu ushirikiano wa vyama vinavyounda Ukawa, Dk
Slaa alisema hilo ni azimio la pili la Kamati Kuu ambayo imebariki
ushirikiano huo kuanzia katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa na Uchaguzi
Mkuu 2015.
“Kamati Kuu imeunda kamati ndogo itakayoongozwa na
Profesa Safari ikiwajumuisha Benson Kigaira, Mnyika na John Mrema
kuangalia namna ushirikiano huo utakavyokuwa. Kamati hiyo imeanza kazi
leo (jana),” alisema.
Alisema azimio la tatu la Kamati Kuu ni
kuhakikisha kuwa Ukawa wanaidai Katiba ya wananchi na kwamba wanatembea
nchi nzima kueleza uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba uliofanywa na CCM
bungeni.
LHRC yawavaa polisi
Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), kimesema Jeshi la Polisi limekurupuka kuzuia wafuasi
wa Chadema kuandamana kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge wakati chama
hicho hakijatoa taarifa rasmi kwa jeshi hilo.
Chapisha Maoni