HOME
 
 
            
Katiba yakoleza kasi urais CCM
Dar es Salaam. Siku chache 
baada ya Bunge Maalumu kupitisha Katiba Inayopendekezwa, mchuano wa 
urais ndani ya CCM umeshika kasi baada ya makada wanaowania nafasi hiyo 
kujihakikishia uzito wa madaraka wanayoyatafuta.
Mjadala wa Katiba ulikuwa umewaweka njiapanda 
makada hao, baadhi wakiwa wameshajitangaza na wengine wakijipanga 
chinichini, huku wakijiuliza wawanie urais upi; wa Muungano, Tanganyika 
au Zanzibar (kwa Wazanzibari), lakini sasa ni kama wamefunguliwa njia.
Hata hivyo, utaratibu wa watu kujitokeza licha ya 
kwamba ni haki yao, umekosolewa ukielezwa kuwa kama hakutakuwa na sifa 
maalumu, mchakato huo unaweza kumalizika kwa kupata mgombea 
asiyestahili.
Wengi wa makada wanaojitokeza na kutajwa ambao 
gazeti hili limewahi kuzungumza nao katika mahojiano maalumu, 
walionyesha wazi kuunga mkono serikali mbili dhidi ya tatu zilizokuwa 
zimependekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph 
Warioba.
Ingawa baadhi yao hawakutaka kuweka bayana, habari
 zilizobainika katika makundi yanayowaunga mkono ni kuwa walikuwa 
wanaona serikali tatu zingeondoa madaraka makubwa aliyonayo Rais wa 
Muungano wa sasa katika muundo wa serikali mbili.
Jambo jingine lililokuwa linawakatisha tamaa 
makada hao ni hoja ya kutaka madaraka ya Rais yapunguzwe kwa kiwango 
kikubwa, iwapo ingepita ingeweza kuwakosesha uwezo wa kulipa fadhila kwa
 wanaowaunga mkono.
“Unadhani nani angetaka kuwa Rais wa Tanzania Bara
 pekee au awe Rais wa Muungano asiyekuwa na mamlaka Bara,” alisema kada 
kundi la mmoja wa wagombea.
Kutokana na hofu hiyo, nguvu za wagombea hao 
zilielekezwa kwanza kwenye Katiba ili kuhakikisha madaraka wanayoyasaka 
yanalindwa, ndipo waanze upya mchuano.
Taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari 
juzi kuwa makundi ya wagombea yalikuwa yanapishana Dodoma kugawa fedha 
kushawishi uungwaji mkono wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), 
zinaelezwa kuwa ni sehemu ya mchuano huo kushika kasi upya.
Kulikuwa na taarifa kuwa ingeibuliwa hoja ya 
kutaka wagombea wengine wabanwe na chama kwa kupiga kampeni, zaidi ya 
lile kundi la makada sita waliokwishapewa onyo kali na chama hicho.
Makada waliopewa onyo hilo ni mawaziri wakuu wa 
zamani, Edward Lowassa (61) na Frederick Sumaye (64) na Waziri wa Mambo 
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (61).
Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano 
na Uratibu), Stephen Wasira (69), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi 
na Teknolojia, January Makamba (40) na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati 
na Madini, William Ngeleja (47).
Wana-CCM wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu 
Mizengo Pinda (66), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel 
Sitta (72), mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla (39), Naibu Waziri wa 
Fedha, Mwigulu Nchemba (39) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi 
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya (65).
Pia yumo mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel 
Nchimbi (43), Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (66), Makamu wa 
Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal (69) na Waziri wa 
Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro (58).
Haki kuonyesha nia
Akizungumzia mbio hizo za urais kwa upande wa CCM 
na vyama vya upinzani, aliyekuwa makamu mkuu wa Chuo cha Mt. Augustino 
Mwanza (Saut), Dk Charles Kitima alisema walioonyesha nia na wanaotajwa 
wana haki kikatiba ya kuongoza nchi.
Alisema pamoja na kwamba wanaojitokeza wana haki, 
utaratibu unaotumika sasa haueleweki tofauti na miaka ya nyuma, vyama 
ndivyo vilivyokuwa vinapendekeza watu watakaogombea.
Alisema utaratibu huo unaonyesha kuwa nchi inakosa
 sifa ya viwango vya juu vya urais kwa kuwa kujitokeza kwa wingi huo 
kunazua maswali mengi na inatia wasiwasi.
Dk Kitima alisema ni lazima kuwe na sifa ya urais kwani atasaidia kwa watu kutokujitokeza au kujitokeza kama ilivyo sasa.
Alisema: “Viongozi wengi wanatafuta urais kwa 
ajili ya uchumi wa familia zao badala ya Taifa, hivyo wananchi lazima 
waeleweshwe.”
 
 
 
 
Chapisha Maoni