Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
TAHARIRI Tanzania bila umasikini sasa inawezekana. KAULI ya Rais Jakaya Kikwet...
TAHARIRI

Tanzania bila umasikini sasa inawezekana.

KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kwamba atakuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini, imeanza kuonekana baada ya Serikali kutoa taarifa ya kuondoa mitambo yote ya kuzalisha umeme inayotumia mafuta na kufunga ya gesi ifikapo Januari mwakani.
Kulingana na taarifa hiyo ya Serikali iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizira ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi jijini Dar es Salaam juzi, kuondoa mitambo hiyo ya umeme, kutaokoa Sh trilioni 1.6.
Hizi ni fedha nyingi ambazo Serikali imekuwa ikipoteza kila mwaka, kwa kuwa na mitambo inayotumia mafuta na sasa fedha hizo zitaelekezwa kwenye masuala ya kijamii, ikiwa ni pamoja na elimu, afya na miundombinu.
Pamoja na faida ambayo wananchi wanaipata kupitia huduma hizo za kijamii, pia umeme huo wa gesi utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama kwa watumiaji, jambo ambalo ni kubwa zaidi, kwani mwananchi anapata faida hiyo moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mitambo wa Kuzalisha Umeme wa Kinyerezi I, Simon Jilima, ujenzi huo umefikia asilimia 75 kukamilika.
Pia, ujenzi wa bomba la kupitisha gesi hiyo mbali na mtambo, nao unakaribia kukamilika kwa asilimia 98 na kwamba ni kilometa tano pekee ndizo zilizobaki, kati ya 542 ya bomba hili zinazotandikwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi I.
Hii ni kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba.
Tunaamini kwamba kukamilika kwa ujenzi wa mtambo na bomba ni hatua kubwa katika kuelekea mafanikio, ambayo Rais Kikwete amekuwa akisisitiza katika siku hizi za hivi karibuni, ambapo anaamini katika kipindi chake, atakuwa ndiye rais wa mwisho kuondoka madarakani nchi ikiwa masikini.
Tumekuwa tukisema hili na tunaendelea kusema kwamba kauli ya Rais Kikwete ina nguvu, si kwa kusubiri hadi hapo atakapokabidhi madaraka baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani, bali mafanikio yake yanaonekana kuanzia sasa.
Hii inatokana na ukweli kwamba hadi Oktoba mwakani uchaguzi utakapofanyika, Serikali ya Awamu ya Nne itakuwa ina mambo kadha wa kadha, ambayo imefanya na ambayo hayahitaji kwenda shule ili kujua undani wake.
Moja ni kuhusu umeme wa gesi, ambao ndio sasa uko kwenye hatua za mwisho kukamilika. Gharama za umeme zimekuwa zikilalamikiwa na watumiaji pamoja na ukweli kwamba ni nishati muhimu kwa maisha ya kila siku.
Serikali ya awamu ya nne imeweza kusambaza na umeme vijijini, ambapo tayari umevuka lengo kabla ya hata mwaka haujaisha kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Lakini, pia mafanikio mengine ni kuhusu elimu, ambapo kila kata sasa ina sekondari.
Pia, Serikali ya Rais Kikwete ina uhakika tatizo la maabara ambalo lilikuwa sugu kwa shule hizi, litakuwa limekwisha baada ya wakuu wa wilaya kusimamia ujenzi wa maabara za masomo yote ya sayansi.
Mafanikio mengine ni katika ujenzi wa barabara, ambapo hivi sasa mikoa yote ya nchi imeunganishwa. Haya yote ni mafanikio makubwa, ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imefanya na haya kama kuna mtu yeyote anabisha, basi mtu huyo ana jambo lake lingine la ziada.

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top