HOME
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Makamanda wa Polisi, Wanasheria wa Serikali, Wafawidhi wa Mikoa na
Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi kabla ya kufungua rasmi Kikao kazi
cha Makamanda hao wa Polisi katika Ukumbi wa Dodoma Convention Center.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
amesimama pamoja na viongozi wengine wakati wimbo wa Jeshi la polisi
ukipigwa. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Charles
Kitwanga, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali George Masaju, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentino Mlowola,
Kushoto kwake ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harison Mwakyembe ,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuph Masauni na
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Ernest Mangu.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili
kwenye ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Convention Center kwa ajili ya
ufunguzi wa rasmi Kikao kazi cha Makamanda hao wa Polisi.
Baadhi
ya Makamanda wa polisi wa Mikoa mbalimbali wakipiga makofi wakati Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa
akiwahutubia.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu kabla ya
kufungua kikao kazi hicho.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akimshukuru Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kufungua
kikao kazi hicho.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika picha ya pamoja na Makamanda wa Polisi wa mikoa mara baada ya
kufungua kikao kazi chao katika ukumbi wa Dodoma Convention Center mjini
Dodoma.
Baadhi ya Makamanda wa polisi wa Mikoa mbalimbali wakiimba Wimbo wa Jeshi la Polisi kabla ya ufunguzi wa Kikao kazi hicho.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mohamed Mpinga.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na
baadhi ya Wanasheria wa Serikali, Wafawidhi wa Mikoa na Wakuu wa
Upelelezi wa Mikoa mara baada ya kufungua kikao kazi cha Makamanda wa
Polisi, Wanasheria wa Serikali, Wafawidhi wa Mikoa na Wakuu wa Upelelezi
wa Mikoa.
PICHA NA IKULU.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka
Jeshi la Polisi nchini na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa
kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 29 Aprili, 2016 wakati
akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili
wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na
Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa
Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.
Awali
kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na
Mawakili Wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili
katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka,
hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo
wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za
hizo.
Kufuatia
kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha
anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha
zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la
Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali
inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.
Ametolea
mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya
kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa
saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza
hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
"Oysterbay
pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye
mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama
majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na
hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za
ghorofa 20 pale, mkaweka investment na Polisi wenu wakakaa pale.
Nimesema
lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya
nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction
ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli
Aidha,
Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya mwendesha Mashitaka wa Serikali
kujipanga kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na
vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya
kuwa na wanasheria mahiri.
"Niwaombe
mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi
mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili
wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa
pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi
inapopelekwa mahakamani wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili
wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote serikali inashindwa.
Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali inashindwa, halafu siku hiyo
unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi"
amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo
zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na
biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa
ujambazi.
Hata
hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango
wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
29 Aprili, 2016
Chapisha Maoni