Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) kwa Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015, leo umewasilisha ripoti yake kamili iliyo na mapendekezo ya marekebisho ya kuboresha mchakato wa uchaguzi na kuongeza imani juu ya chaguzi zijazo, kwa washirika wake nchini.
Uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, uliyofanyika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulionyesha dhamira ya Watanzania ya kuzingatia mfumo wa kikatiba na pia kuheshimu misingi ya kidemokrasia. Chaguzi zote mbili za tarehe 25 Oktoba, yaani za Muungano na Zanzibar, zilikuwa na ushindani mkali na kwa kiasi kikubwa ziliendeshwa vyema. Taasisi za usimamizi wa uchaguzi zilionyesha viwango vya kutosha vya kujiandaa pamoja na uwezo wa kuendesha hatua muhimu katika kuandaa uchaguzi, kuelekea na pia siku ya uchaguzi.
Kulikuwepo, hata hivyo, na mapungufu kadhaa yanayopaswa kuangaliwa kuhusu mfumo wa kiuchaguzi pamoja na utendaji wa mchakato wa uchaguzi kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Zaidi ya hayo, taasisi za usimamizi wa uchaguzi hazikuonyesha uwazi kamili juu ya michakato yao ya kufanya maamuzi.
Tathmini chanya juu ya kuaminika kwa uendeshaji wa uchaguzi siku ya uchaguzi ilihusu pia Zanzibar. Kufuatia uamuzi wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar, EU EOM pamoja na waangalizi wengine wa kimataifa, katika tamko la pamoja, walielezea wasiwasi wao mkubwa na kuiomba ZEC iwasilishe ushahidi wa kuhalalisha uamuzi huo ambao haujawahi kutokea. Ushahidi huo haujawahi kuwasilishwa. EU EOM haikufanya uangalizi wa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016 Zanzibar kwa kuwa iliona ya kwamba mazingira hayakupelekea uchaguzi shirikishi, halisi na wa kuaminika.
Muangalizi Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa EU, Bi Judith Sargentini, Mbunge wa Bunge la Ulaya, amerejea Dar es Salaam wiki hii ili kuwasilisha ripoti kamili kwa NEC, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vyama vya siasa pamoja na vikundi vya uangalizi vya kitaifa.
Mapendekezo yaliyo ndani ya ripoti hiyo, ambayo baadhi yaliwasilishwa pia mwaka 2010, ni pamoja na haki ya wagombea binafsi kugombania katika uchaguzi wowote wa Muungano au Zanzibar; kuruhusu haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais kisheria; haki ya vyama vya siasa kuunda umoja wa kiuchaguzi; kuangaliwa upya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015; kuendelezwa kwa muundo wa kudumu wa NEC katika ngazi za mikoa, na marekebisho ya mchakato wa uteuzi wa makamishna wa uchaguzi wa NEC na ZEC; na kuangaliwa upya mchakato wa uandikishwaji wa wapiga kura Zanzibar ili kuhakikisha ushirikishi zaidi pamoja na imani ya wapiga kura.
“Nina furahi sana kuwasilisha ripoti yetu kamili leo kwa kuwa inajumlisha yote tuliyoyaona wakati wa uangalizi wetu katika kipindi cha miezi mitatu ambapo ujumbe umekuwepo nchini, pamoja na mapendekezo ya kina kwa chaguzi zijazo. Umoja wa Ulaya unaendelea kusimamia dhamira yake ya kufanya kazi na washirika wake Tanzania kuimarisha mchakato wa kidemokrasia nchini, na utaendelea kutazama kwa karibu marekebisho ya kiuchaguzi nchini katika miezi na miaka ijayo,” alisema Bi Sargentini katika mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Ripoti inatoa mapendekezo muhimu ya kufikiriwa na mamlaka husika, taasisi za usimamizi wa uchaguzi pamoja na wadau wengine wa uchaguzi. Mapendekezo hayo ni pamoja na yafuatayo:
Mfumo wa Kiuchaguzi:
Kuruhusiwa kwa haki ya kugombania kama mgombea binafsi kwa ajili ya uchaguzi wowote wa Muungano au Zanzibar;
Kuwepo kwa haki ya kulalama matokeo ya uchaguzi wa rais katika sheria;
Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 itumike kwa uwiano ili kulinda haki ya kujieleza na
haki ya kuwa na kesi isiyo na upendeleo;
Utendaji wa Uchaguzi:
Kuangaliwa upya mipaka ya majimbo ili kuhakikisha usawa zaidi wa kura;
Muundo huru na wa kudumu wa NEC katika ngazi za mikoa;
Mabadiliko katika taratibu za uteuzi wa makamishna wa NEC na ZEC ili kuongeza imani
juu ya uhuru wao;
Uandikishwaji Wapiga Kura:
Kipindi kirefu zaidi cha kuonyeshwa orodha za wapiga kura za Muungano na Zanzibar;
Kuangaliwa upya mchakato wa uandikishwaji wapiga kura Zanzibar ili kuhakikisha imani
na ushirikishi zaidi;
Elimu kwa Wapiga Kura:
• Mazoezi ya elimu kwa wapiga kura yaliyoandaliwa vyema na kutekelezwa kwa wakati toka tume za uchaguzi;
Vyombo vya Habari:
Kubadilishwa kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuwa mashirika ya utangazaji ya huduma kwa umma;
Marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya 2003 ili kuhakikisha uhuru wa TCRA;
Upigaji kura, kuhesabu na kuorodheshwa kwa matokeo:
• Kuboreshwa kwa mafunzo ya maafisa uchaguzi na watendaji wa vituo kuhusu taratibu;
Malalamiko na Rufaa:
• Maamuzi ya NEC na ZEC yaweze kupingwa mahakamani kipindi kizima cha mchakato. Wanaolalamika wasilazimishwe kusubiri hadi matokeo kutangazwa ili kutafuta njia ya kupata haki.
EU EOM ilikuwepo nchini kati ya tarehe 11 Septemba na 8 Desemba 2015, kufuatia mialiko toka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzaibar.
Kwa ujumla, ujumbe ulituma waangalizi 141 nchini kote, toka Nchi zote 28 Wanachama wa EU, pamoja na Norway, Uswisi na Canada, na kuufanya kuwa ujumbe mkubwa kabisa wa waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi huo. Ujumbe ulitathmini ni kwa kiasi gani mchakato wa uchaguzi ulizangatia ahadzi za kitaifa na za kikanda kuhusu uchaguzi, pamoja na sheria za Tanzania.