Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME JICHO LANGU: Sheria butu, madereva kanjanja UNASHANGAA nini? Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! ...
HOME

JICHO LANGU: Sheria butu, madereva kanjanja

UNASHANGAA nini? Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni!
Kijana mmoja ana ulemavu wa kusikia na kuongea (bubu). Kafikiria sana, kaona kazi ya bodaboda ndiyo ya kumwingizia kipato. Sasa anafanya kazi hiyo. Anasafirisha abiria kwa pikipiki kwenda maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Usiniulize akipigiwa honi barabarani anajuaje! Wala usiniulize anawasilianaje na abiria akiwa amempakia. Hayo maswali nenda kaulize mamlaka zenye jukumu la kusimamia usalama wa barabarani.
Unashangaa huyu bubu kuendesha pikipiki! Mbona hushangai ‘mateja kuendesha daladala?. Nani asiyefahamu daladala nyingi hususani jijini Dar es Salaam, hukabidhiwa kwa wapiga debe waliobatizwa jina la ‘day worker’ ambao wengi wao ni wavuta unga?
Kutokana na uhuru uliopo, usije kushangaa unakutana na mtoto wa chekechea akiendesha daladala, bodaboda au hata basi la abiria la masafa marefu. Utashangaaje wakati udereva sasa unachukuliwa poa?
Cha msingi, ufahamu kuwasha gari, kushika usukani, kukanyaga mafuta na kushika breki. Unajifunza leo gari, kesho unaingia barabarani na kupakia abiria. Kwa mtindo huu, kwa nini ajali zisiendelee kupukutisha maisha ya watu?
Hivi karibuni zimeshuhudiwa ajali mfululizo zikihusisha mabasi ya abiria ambazo katika uchunguzi wa awali, unakuta tatizo ni kutozingatia kanuni. Kanuni za barabara zinazohusisha sheria na ushauri wa namna ya kutumia barabara , zipo.
Lakini ni kama madereva hawazielewi. Kiburi na ubabe vimeendelea kutawala. Hakuna ubishi, ubabe na kiburi wa madereva, vinatokana na adhabu kuwa ndogo kiasi cha kutoogopwa.
Adhabu zinazotolewa kwa wavunjaji wa sheria barabarani, hazitishi wala kuogofya wahalifu. Unategemea dereva atakuwa na hofu kama kosa la usalama barabarani anatozwa faini ya Sh 100,000! Au dereva ataogopaje kama adhabu ni kunyang’anywa leseni ?
Hata akinyang’anywa, si atazunguka mlango wa nyuma, atahonga na kupewa leseni nyingine kwa jina lingine? Hata kama atakwenda jela, jiulize ni miaka mingapi kama si miaka isiyozidi mitano.
Eti hiyo ndiyo adhabu ya mtu aliyekiuka sheria na kusababisha ajali inayogharimu maisha ya makumi ya watu. Umefika wakati wa kutafakari adhabu zinazotolewa kwa watu wanaosababisha ajali barabarani.
Bila sheria kuangaliwa upya, ushauri kwa madereva kuhakikisha hawanywi pombe na kuendesha, utaendelea kupuuzwa. Aidha fujo za madereva kujaribu kupita walio mbele, hazitakoma.
Ndiyo maana katika ajali nyingi zinazotokea nchini, wengi huangukia kwenye kosa hili. Hahitaji elimu ya digrii kwa dereva kutambua kwamba kabla ya kupita gari lingine, lazima ajiridhishe kwamba upo upenyo mkubwa wa kutosha mbele ya gari unalotaka kupita.
Lakini kiburi na ubabe vimetawala barabarani, wengi hawatekelezi. Sheria za madereva ziko wazi kwamba lazima awe na leseni halali ya udereva kwa daraja la gari analoendesha.
Anashauriwa aendeshe gari akiwa katika afya nzuri kwa maana asiwe mgonjwa au amechoka, aone vizuri kwa maana aweze kusoma kibao cha namba za gari kutoka umbali wa meta 20.
Zaidi dereva anashauriwa anapojisikia kuchoka wakati wa kuendesha, atafute sehemu salama ya kusimama na kupumzika. Anapaswa apumzike kwa dakika 30 kila baada ya kuendesha kwa saa tatu. Hapaswi kuendesha kwa zaidi ya saa tisa kwa siku.
Sasa nieleze, ni madereva wangapi wa masafa marefu, hasa mabasi ya abiria, wanaozingatia hili? Mbona yanashuhudiwa mabasi yakiwa na dereva mmoja tangu alfajiri hadi usiku wa manane bila mapumziko. Kwa mtindo huo, ajali zitakoma?
Madereva wamekuwa wakipuuza ushauri kwa kuendesha vyombo vya moto kwa kasi kubwa katika namna ambayo haiwawezeshi kusimama ghafla kuepuka kugonga kitu chochote.
Huwa inashangaza kuona dereva akiendesha kwa kasi kwenye kona au juu ya kilele cha mlima ambako ni vigumu kuona iwapo kutakuwapo gari lililoharibika mahali.
Hushindwa kuzingatia kwamba, dereva akiongeza maradufu mwendo wa chombo, umbali wa kusimama unaongezeka. Alama za pundamilia ndio kabisa zimegeuzwa mapambo barabarani kutokana na madereva kutoziheshimu.
Naamini wageni wanaotoka nchi zenye ustaarabu na zinazozingatia sheria za barabarani, huwa wanashangaa. Lazima washangae kushuhudia madereva wakipigia wavuka kwa miguu honi kwenye alama za pundamilia kana kwamba hawana haki ya kuvuka barabarani.
Tena hushangaza kuona utovu huu wa nidhamu barabarani ukifanywa na wasomi, viongozi ambao hutembelea nchi nyingine na kushuhudia ustaarabu barabarani.
Kwa ujumla, usafiri wa barabarani umetawaliwa na madereva ‘makanjanja’ huku udhibiti wao ukiwa wa mashaka. Sheria zingekuwa kali kiasi cha kutoa adhabu kali, ujinga, ubabe na kiburi cha madereva vingedhibitiwa.
Hata kama kanuni zipo, bila sheria kali, zitaendelea kukiukwa na hivyo kufanya usafiri wa barabara kutokuwa salama, badala yake kuwa wa mashaka.
VIA HABALI LEO

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top