HOME
Kura za Zanzibar ni pasua kichwa
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hadi jana,
ni wajumbe 143 tu kati ya 219 kutoka upande huo waliokuwa wamepiga kura,
huku wajumbe 86 wakiwa bado hawajatimiza haki yao hiyo ya kidemokrasia.
Kati ya wasiopiga kura, 66 ni wajumbe wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao walisusia Bunge hilo Aprili 16, mwaka
huu kutokana na kile walichodai kuwa ni kutoridhishwa na jinsi Bunge
linavyoendeshwa, wakati wajumbe 20 hawajapiga kura kutokana na sababu
mbalimbali zikiwamo za kwenda kuhiji Saudi Arabia.
Jana asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel
Sitta alisema licha ya njama zinazofanywa na watu kukwamisha rasimu hiyo
isipate kura za kutosha, mipango yao haitafanikiwa kwani kulikuwa na
kila dalili kwamba kazi hiyo ingehitimishwa kwa ufanisi.
Hata hivyo, uchambuzi wa kitakwimu unaonyesha kuwa
kulikuwa na kila dalili ya kukosekana kwa theluthi mbili ya kura
zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria kwa upande wa Zanzibar kwani kati ya
143 ya waliopiga kura, saba kati yao walipiga kura ya ‘hapana.’
Kadhalika, wajumbe wawili akiwamo Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman walipiga kura
wakikataa baadhi ya ibara, wakati kura za ‘ndiyo’ zilikuwa 105.
Kitendawili kinachosubiriwa kilikuwa ni kuhusu
kura 30 za siri ambazo hadi jana matokeo yake yalikuwa hayajawekwa wazi,
huku kukiwa hakuna taarifa zozote kuhusu kura zilizotarajiwa kupigwa na
wajumbe 20 ambao hawapo Dodoma.
Awali, kulikuwa na mpango wa kuwawezesha wajumbe
hao kupiga kura huko waliko na uongozi wa Bunge Maalumu ulikusudia
kupeleka ofisa wake, Makka, Saudi Arabia ili kuwawezesha wajumbe wake
wanane ambao ni mahujaji kupiga kura wakiwa huko.
Ili kupata theluthi mbili, zinatakiwa kura 146,
idadi ambayo kutimia kwake kwa mujibu wa takwimu zilizopo hadi sasa
zinatakiwa kura nyingine za ‘ndiyo’ 14.
Kwa maana hiyo hata kama kura zote za siri 30
zitaunga mkono rasimu hiyo, bado haziwezi kuiwezesha kupata kura
zinazotakiwa kwani zitafikia 135, hivyo kuendelea kuwapo pengo la kura 9
ili kufikisha kura 146.
Msako wa kura
Kutokana na mazingira hayo, habari zilizolifikia
gazeti hili juzi na jana zinasema kulikuwa na jitihada kubwa za
kuwashawishi baadhi ya wabunge wa Ukawa wapige kura.
Waliotajwa kulengwa na mpango huo ni wabunge wa Viti Maalumu
(Chadema) kutoka Zanzibar, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Abama ambao
jana kwa nyakati tofauti, walithibitisha kusakwa.
“Kweli nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi
kuwataja na wananitaka nipige kura na wengine walifika mpaka nyumbani
lakini mimi siwezi kushiriki maana nikifanya hivyo dhamiri yangu
itanishtaki,” alisema Msabaha.
Abama alisema: “Nimepewa alert (ilani) na viongozi
wangu kwamba nasakwa, kwa hiyo nimekaa ndani tu wala sitoki maana sina
uhakika hao wanaonisaka wana malengo gani. “Hata simu sipokei anapokea
mume wangu tu, sema tu kwamba hivi katoka hivyo ilipoingia nikasema basi
ngoja nipokee, lakini jambo moja ni kwamba hata kama hao wanaonitafuta
wangenipata, siwezi kushiriki kupiga kura kwa kitu ambacho sijashiriki
kukiandaa.”
Jana, Sitta alitoa taarifa bungeni akisema kuna
wajumbe wawili waliokuwa wamegomea Katiba hiyo na kwamba baada ya kusoma
rasimu inayopendekezwa wamekubali kupiga kura.
“Mmoja amekubali kupiga kura na anasema yuko
tayari hata kufukuzwa na chama chake, sasa wale wanaotumia mbinu za
ovyoovyo ili mchakato huu usikamilike wanapoteza muda, maana ukizuia
maji huku, yanaelekea kwenye mkondo mwingine,” alisema.
Sitta alikuwa akizungumzia mchakato wa upigaji
kura huku akirejea ujumbe alioandikiwa na Mwanaidi Othman Tahiri ambaye
alilalamika kwamba jina lake limerukwa na baadaye alipiga kura ya
‘hapana.’
“Mwenyekiti wake wa chama cha NRA, alikuwa
ameniandikia kuwa mjumbe huyo alipopiga kura ya ‘hapana’ alikuwa
hakuelewa maana yake, kwa hiyo alisema pengine tukae naye aweze
kuelimishwa vizuri,” alisema Sitta.
Alisema mjumbe mmoja ambaye jina lake
analihifadhi, alikuwa akimshikilia Mwanaidi kama mfungwa wake na alikuwa
akifanya kazi kubwa ya kuhakikisha zinapigwa kura za ‘hapana’ kutoka
Zanzibar.
Vitisho
Sitta pia alidai kwamba baadhi ya wajumbe juzi waliokolewa na uongozi baada ya kuzuiwa hotelini mwao ili wasiende kupiga kura.
“Jana (juzi), ilibidi tutumie mamlaka za kiusalama
kumkomboa mjumbe aliyekuwa amefungiwa hotelini ili asije kupiga kura,
hatimaye tuliweza kumkomboa na akaja kupiga kura ya siri,” alisema
Sitta.
Katika tukio la pili, alisema kuna wajumbe wawili
juzi walifika kwa Katibu wa Bunge hilo na kuonyesha ujumbe mfupi wa simu
za mkononi (sms), wenye vitisho na kwa kuwa waliogopa ilibidi Katibu
awaruhusu kuondoka... “Wametishwa sana kwamba wasiendelee kubaki hapa
Dodoma na sasa wameondoka, lakini vitisho pia ni jinai.”
Alihoji watu wa aina hiyo wanachokitafuta hadi kutumia mbinu alizoziita za kimafia wana lengo gani na nchi yao.
Alihoji watu wa aina hiyo wanachokitafuta hadi kutumia mbinu alizoziita za kimafia wana lengo gani na nchi yao.
Chapisha Maoni