KURUDISHWA nyumbani katika muda mfupi wa saa 24 kwa wanafunzi wa 7,802 wa Stashahada maalumu ya ualimu wa masomo ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kumewaunganisha wabunge wa CCM na upinzani katika kuwatetea, kiasi cha kulazimisha shughuli za Bunge kuahirishwa kabla ya wakati.
Kabla ya wabunge hao kuchachamaa kuwatetea wanafunzi hao, Serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ilitoa taarifa ya wanafunzi hao kutakiwa kurejea makwao ndani ya muda huo mfupi.
Taarifa ya serikali
Katika taarifa hiyo ya Serikali, Profesa Ndalichako alisema hatua hiyo imetokana na mgomo wa wahadhiri wa chuo hicho, ambao walikataa kufundisha wanafunzi hao kwa takribani mwezi mmoja sasa.
Sababu za mgomo huo kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, ni madai ya fedha ya walimu hao kwa Serikali ambayo hayakufafanuliwa, lakini kiwango cha madai hayo kilikataliwa na mkaguzi wa ndani wa Udom.
Kukataliwa kwa kiwango hicho, kulikofanywa na mkaguzi wa ndani wa Udom, ndiko kulikosababisha mgomo huo, ambao Profesa Ndalichako alisema Serikali ilijaribu kuingilia kati kwa karibu mwezi mmoja bila mafanikio.
“Hawa walimu (wahadhiri) wana madai ambayo mkaguzi wa ndani anasema si sahihi na mnajua masuala ya fedha, Serikali haiwezi kumuingilia mkaguzi…tutaangalia namna ya kuwapatia fursa ya mafunzo yenye tija kwa wanafunzi hawa,” alisema Profesa Ndalichako.
Bunge latibuka
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) ndiye alianza kwa kuomba mwongozo, ambao baada ya kuruhusiwa alisema wanafunzi hao waliorudishwa nyumbani, hawana makosa na wengi wametoka maeneo mengi nchini.
“Waliogoma ni walimu, adhabu wanapewa wanafunzi, kwa nini Serikali isimalize tatizo la walimu wachache badala ya kuadhibu wanafunzi wengi? Jana, wanafunzi hawa walikuwa wakizurura maeneo yote ya Dodoma, ni watoto wasichana na wavulana, hatujui hata kama wamelala usiku. “Kama mkaguzi kasema hakubaliani na fedha, kwa nini msiwaite na kukubaliana, naomba kutoa hoja, Bunge hili liahirishe shughuli zinazoendelea ili kujadili suala hili la dharura,” alisema na kuungwa mkono na wabunge wote wa upinzani na CCM, huku wakishangilia kibunge.
Naibu Spika
Akijibu muongozo huo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, alianza na kuelezea masikitiko yake binafsi kwa kilichotokea kwa wanafunzi hao, lakini akasema kwa kuwa Waziri ameshalitolea taarifa, maana yake Serikali inayo taarifa.
Mbali na tamko la Serikali kuonesha kuwa na taarifa, Dk Tulia alisema pia Bunge halina taarifa za kutosha kuliwezesha kujadili suala hilo, akitoa mfano taarifa ya mkaguzi huyo wa ndani.
Sababu nyingine ya kuzuia mjadala huo, Dk Tulia alisema ni kukosewa kwa matumizi ya kanuni aliyotumia Nkamia, kwa kuwa awali alitaja Kanuni ya 68 kanuni ndogo ya saba kuomba mwongozo, akaruhusiwa na Naibu Spika.
Hata hivyo baada ya kuomba mwongozo, Nkamia aliomba mjadala uliokuwa ukiendelea uahirishwe ili kutoa nafasi ya hoja hiyo ya Udom kujadiliwa, jambo alilopaswa kuomba baada ya kutamka Kanuni inayotumika katika ombi hilo ya 69 na udharura wa hoja hutawaliwa na Kanuni ya 47, lakini hakufanya hivyo na kujikuta akikosa uhalali wa ombi hilo la pili.
Wakaidi kiti
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, wabunge wote wa upinzani na CCM, waliendelea kupiga kelele, wengine wakiomba muongozo na wengine utaratibu, jambo lililosababisha Naibu Spika kuwataka wakae chini.
Kwa kuwa aliyekuwa ametoka kuzungumza alikuwa mbunge kutoka CCM, Dk Tulia alitoa nafasi kwa upinzani, iliyokwenda kwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari ambaye alisahihisha kosa lililofanywa na Nkamia na kurejesha hoja ile ile bungeni na kuungwa mkono na wabunge karibu wote wa upinzani na sehemu ya wabunge wa CCM.
Nasari katika kurejesha hoja hiyo, alitaja Kanuni hiyo ya 69, ambayo haikutajwa na Nkamia, ili hoja hiyo ya kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi wa Udom, ijadiliwe bungeni.
Hata hivyo, Naibu Spika alitumia kanuni hizo hizo, hasa ya 68 sehemu ndogo ya pili; inayomwezesha Spika kupima kama kuwasilishwa kwa hoja husika ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge; na Kanuni ya 47 sehemu ndogo ya nne, inayomwezesha kupima udharura wa hoja na kama ina maslahi kwa umma.
Baada ya kusoma kanuni hizo, Dk Tulia alisema haoni kama hoja hiyo inakidhi vigezo vya uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na pia haoni kama ina udharura unaozungumzwa.
Wabunge watolewa nje
Kauli hiyo ya Dk Tulia, ilisababisha wabunge waliokuwa wakiunga mkono hoja hasa karibu wote wa upinzani kusimama na baadhi ya wabunge wa CCM, waliokuwa wakiunga mkono hoja hiyo, nao kusimama huku wakiendelea kuongezeka kusimama.
Kutokana na hali hiyo, Dk Tulia huku akiwa amesimama, aliagiza wabunge wote waliosimama wakae chini, lakini agizo hilo halikutekelezwa na badala yake, baadhi ya wabunge wa CCM, walianza kusimama kuungana na wa upinzani. Dk Tulia alirudia agizo lake mara ya pili na ya tatu; akaagiza askari wa Bunge waingie na kuwatoa nje wabunge wote waliosimama wakiwemo wa CCM.
Wakati askari hao wakiingia kukabiliana na wabunge hao, Naibu Spika aliahirisha shughuli za Bunge kabla ya muda wa kawaida ambao ni saa 7 mchana. Badala yake aliahirisha shughuli saa 5 asubuhi, muda ambao wabunge walipaswa kuendelea kujadili hoja ya bajeti ya Wizara ya Maji.
Miongoni mwa wabunge wa CCM waliokuwa wamesimama ni pamoja na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Nkamia mwenyewe, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Simba, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola na wengine ambao walikuwa wakiongezeka kusimama wakati Naibu Spika ameshaagiza waliosimama kutoka nje.
Kamati zakaa Mbali na kuahirisha shughuli za Bunge kabla ya wakati, Naibu spika aliagiza Kamati ya Uongozi kukutana bila kueleza ajenda za kamati hiyo, hali iliyotafsiriwa kuwa kamati hiyo inakwenda kujadili sintofahamu hiyo ya Udom.
Mbali na kamati hiyo, Kamati ya wabunge wa Kambi ya upinzani ilitangazwa mapema kuwa itakutana hata kabla ya kuibuka kwa hoja hiyo ya Udom, jambo lililoonesha kuwa suala hilo litachukua nafasi katika mjadala wake.
Taarifa iliyofikia gazeti hili kutoka kwa baadhi ya wabunge wa CCM, Kamati ya Wabunge wote wa CCM, nayo iliitishwa mara baada ya kuahirishwa kwa Bunge kabla ya wakati, hali iliyoonesha kuwa ajenda kuu wa Kamati hiyo ya Wabunge wa CCM, itakuwa suala la Udom.
Siasa za upinzani
Katika hatua nyingine, wabunge wa upinzani wakiongozwa wa Nasari, walitengeneza mazingira ya kubeba hoja hiyo kisiasa zaidi, ambapo mbunge huyo wa Arumeru Mashariki, alikabiliana na askari wa Bunge, walioamua kumsukuma kutoka nje, wakati Naibu Spika akiwa ameshaahirisha shughuli za Bunge.
Walipotoka nje, wabunge hao wa upinzani walikwenda kuzungumza na waandishi wa habari huku wengine wakitoa machozi.
Baada ya muda, Nasari akiwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) alirejea walipokuwepo waandishi na kusema wabunge walikesha stendi ya mabasi ya Dodoma kubeba wanafunzi hao, kwa kuwa hawakuwa na pahali pa kwenda na wabunge ndio walikuwa kimbilio lao.
Hali hiyo ya wabunge wa upinzani ilisababisha Nkamia aliyekuwa karibu na walipokuwa waandishi wa habari waliokuwa wakiwasikiliza wabunge hao wa upinzani kusema; “hoja nimeianzisha mie, kuhojiwa wanahojiwa hao (wapinzani)” huku akiondoka kwenda katika Ukumbi wa Msekwa, ambako kulitarajiwa kufanyika kwa vikao vya vyama.
Chapisha Maoni