HOME
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA NCHINI TANZANIA AKIHUTUBIA WAJUMBE MUDA MCHACHE BAADA YA BUNGE HILO KUNZA KAZI YAKE TENA
HOTUBA YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA NCHINI TANZANIA AKIHUTUBIA WAJUMBE MUDA MCHACHE BAADA YA BUNGE HILO KUNZA KAZI YAKE TENA
Karibuni
tena Dodoma Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la kutunga Katiba ya
nchi yetu. Sote tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu kwa
kuendelea kutupa uhai na afya hadi leo kutuwezesha kuwepo ndani ya
ukumbi huu. Tupo humu ili tuitekeleze kazi waliyotukabidhi Watanzania
wenzetu milioni arobaini na sita (46) ya kuwapatia Katiba mpya. Dhamana
hii ni nzito na haistahili kufanyiwa ajizi.
Tunaendelea na shughuli zetu za Bunge Maalum kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema
“Akidi
kwa kila kikao cha Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha uamuzi wa
Bunge Maalum itakuwa ni nusu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum“.
Nimetaarifiwa
na Katibu kwamba wajumbe waliokuja Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo
tatu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum. Nawashukuruni nyote kwa kuja hapa
Dodoma ili kutimiza wajibu wenu.
Kwa
niaba yenu, nawashukuru Watanzania wenzetu wote ambao kwa mamilioni
wamedhihirisha utashi mwema wa kisiasa kwa kuunga mkono hatua ya Bunge
Maalum kuendelea na kazi zake hadi tuipate Katiba inayopendekezwa ambayo
wataipigia kura ya maoni. Kipekee na kwa niaba yenu, nawashukuru kwa
dhati viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wanaloliombea Taifa hili
mafanikio Bunge Maalum, wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi na
umoja ndani ya nchi na siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
Kwa
leo sikupenda sana kuzungumzia hoja mbali mbali zinazotawala magumzo ya
mchakato wa Katiba mpya hapa nchini, magumzo yanayoendeshwa na makundi
maalum kwa jazba na hata matusi. Hata hivyo nalazimika kutoa maelezo ya
ufafanuzi kuhusu upotoshaji mkubwa unaoendeshwa na baadhi ya watu kuhusu
Bunge Maalum. Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao wajibu wa kuwafafanulia
wananchi kuhusu uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea na
utaratibu wa shughuli zetu.
Ni Rasimu ya Tume au la
Wapo
wanaodai kuwa eti hapa Bungeni hatujadili Rasimu ya Tume. Tuhuma hii
haina ukweli hata kidogo. Msingi wa majadiliano yote tangu tumeanza ni
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba. Utaratibu ni kwamba
pale ambapo wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa wanafanya hivyo. Maana
ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya
taasisi ya juu zaidi. Anayekabidhiwa rasimu anayo haki na mamlaka ya
kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu. Itakuwa ni jambo
la ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya
kujadili Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati
ilipowasilishwa!
Je suala ni muundo wa Muungano tu?
Maudhui ya Rasimu yanajumuisha baadhi ya masuala muhimu yafuatayo:
- Kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora zaidi wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano
- Kuimarisha haki za binadamu ili kuwawezesha raia wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia bila ubabe na dhuluma
- Kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa bila kujali maslahi ya wengi na ya vizazi vijavyo.
- Kujenga uwiano sahihi na wenye haki baina ya wanawake na wanaume katika nafasi za uongozi.
-
Kubainisha hatua zenye kuleta matumaini mapya ya maendeleo kwa makundi
maalum ya vijana wakulima wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi
za kawaida, walemavu, wafanya biashara wadogo na wajasiriamali
wengine.
-
Kuweka msingi imara wa kutungwa kwa sheria kakamavu za kuzuia
ukandamizaji wa raia, unyonyaji, wizi wa mali ya umma, rushwa,
hujuma dhidi ya uchumi na kuzuia mapato haramu na fedha chafu.
- Kutambua haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali wengine ili kupunguza migongano na migogoro.
- Kuweka Misingi ya utawala bora inayozingatia uadilifu, sifa stahiki na ufanisi.
-
Kuwezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi zitakazosimamia chaguzi
zilizo za haki na huru zaidi pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi
zilizoboreshwa.
Zaidi
ya hivyo, yapo mapungufu katika Rasimu iliyopo kwa kuachwa masuala ya
kuwezesha Serikali za mitaa; kutoa maelekezo kuhusu masuala ya matumizi
ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa. Nini kinatuzuia kuiboresha
Rasimu kwa kuyaongeza mambo haya ndani ya Katiba kwa faida ya Taifa?
Yote
haya ni masuala muhimu ambayo yamo ndani ya rasimu na wakati wake wa
kuyaweka sawa ndiyo huu. Pamoja na umuhimu wake suala la muundo wa
Muungano si suala la kutulazimisha tuyaahirishe mazuri yote yaliyomo
katika Rasimu tuliyopewa.
Uhalali wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja
na uhalali wa kisheria wa Bunge hili Maalum kuendelea kufanya kazi
zake, linao pia uhalali wa kisiasa kutokana na sifa za uwakilishi wetu
na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu. Kutofautiana maoni hakuwapi
hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele ya
wananchi kuliko wenzao. Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura na
wa maridhiano. Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi
wa jamii wa kususia mijadala halali na kwenda nje kuelezea hoja za
upande mmoja hauna nafasi katika Tanzania jamii isiyotaka fujo na
utengano.
Wajumbe
wa Bunge Maalum wanaoendelea na kazi mjini Dodoma ni wateule wa Rais
kwa niaba ya wananchi kwa kazi ya kutunga Katiba. Kazi hii haiwezi
kusitishwa kwa sababu tu wajumbe wachache wameisusia. Tutazingatia
matakwa ya sheria katika kufikia hatma ya mchakato wa Katiba.
Mabadiliko ya Kanuni
Kama
nilivyoeleza hapo mwanzo, Rasimu ina jumla ya sura kumi na saba (17)
zenye mambo mengi yenye maslahi kwa Watanzania wote. Kwa muda tuliopewa
wa siku sitini (60) isingewezekana kuikamilisha kazi tuliyopewa ndani ya
muda. Ikumbukwe kwamba kwa Kanuni zilivyo, kila sura mbili zinahitaji
siku tisa kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua siku takriban mia
moja thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii! Pendekezo la msingi
hapa ni kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili
sura kumi na tano (15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura
mbili zilizojadiliwa awali na ikibidi ziongeze sura ambazo zitadhihirika
kuwa ni muhimu. Naamini mtiririko huu utatuwezesha kuwa na mpangilio
bora zaidi wa sura na ibara katika Katiba mpya. Tusingependa na wala
isingefaa kuomba tena muda wa ziada wa kazi ya Katiba ndio maana
tunafanya mabadiliko ya Kanuni. Kamati ya Uongozi iliyoketi Dar es
Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza yafanywe mabadiliko ya Kanuni
za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda tuliopewa. Kwa
hiyo nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na
hatimaye kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba
muikubali ratiba iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni
kwa lengo nililolieleza hapa.
HITIMISHO
Pamoja
na maoni ya kila namna yanayoendelezwa kujadili mchakato wa Katiba nje
ya Bunge hili, ni muhimu wahusika wapunguze jazba, chuki na upotoshaji.
Bunge Maalum lisaidiwe kwa mawazo chanya ili limalize kazi yake.
Sisi
tuliomo humu katika Bunge Maalum tuna wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa
umakini na kwa uadilifu ili kazi yetu iwe bora. Tujadiliane kwa
uungwana. Tofauti za mawazo zisitufanye tuingize chuki na maneno
yasiyofaa. Katika mabadiliko ya Kanuni nashukuru sasa Kiti kimepewa
mamlaka ya kushughulikia utovu wa nidhamu ndani ya wakati. Lakini
ninaamini haitakuwa lazima kwangu mimi au Makamu Mwenyekiti kutumia
nguvu za mamlaka yetu ila tu pale itakapobidi.
Nawatakia nyote Mkutano wenye mafanikio kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!
Samuel Sitta – MB
MWENYEKITI BUNGE MAALUM LA KATIBA
Chapisha Maoni