HOME
Afrika ipigane kutokomeza umasikini
- AKIWA ziarani nchini Marekani, Rais Jakaya Kikwete amesema pamoja na changamoto nyingi ambazo Bara la Afrika inakumbana nazo, bado kuna uwezekano wa kuondoshwa kwa umasikini katika bara hilo.
Akitoa hotuba kwenye mkutano unaojadili
Maendeleo na kumaliza Umasikini, ulioandaliwa na Shirika la Misaada la
Marekani (USAID), jijini Washington juzi, Rais Kikwete alisema Afrika
ikiwa na sera sahihi na ushirikiano mzuri baina ya serikali na sekta
binafsi, umasikini utaondoka.
Akiunga mkono kauli hiyo ya Rais
Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alimwelezea
Rais Kikwete kuwa ni kiongozi mtendaji na ambaye amechangia katika
kuleta amani katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na kukuza utawala
bora nchini Tanzania.
Mathalani, akiizungumzia Tanzania, Rais
Kikwete alisema mafanikio ya kiuchumi yameanza kuonekana baada ya
kutangazwa kwa mageuzi ya kiuchumi kwenye miaka ya 1980, mageuzi ambayo
yamedumu na kuonesha mafanikio makubwa hadi sasa.
Alisema kupitia mageuzi hayo, uchumi
umekua kutoka asilimia 3.5 mwaka 1990 hadi kufikia kiwango cha asilimia 7
katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Hata hivyo, alisema kiwango hicho cha
uchumi bado hakiridhishi kwa sababu sekta muhimu ya kilimo ambayo ndiyo
inayotoa ajira kwa Watanzania wengi, haijakua na kuendelea vya kutosha
na badala yake sekta zinazohusika na utoaji huduma, mawasiliano, ujenzi,
uzalishaji na madini ndizo zimekua zaidi.
Tuonavyo sisi, ni ukweli ulio wazi
kwamba Bara la Afrika lina uwezo mkubwa wa kuondosha umasikini pamoja na
changamoto mbalimbali zinazolikabili bara hilo, endapo kutakuwa na
mikakati madhubuti.
Tunasema hivyo kutokana na mafanikio
ambayo yameanza kujitokeza katika Mataifa mbalimbali ya Afrika baada ya
kuzifanyia mageuzi makubwa Sera zao zinazosimamia ukuzaji uchumi na hasa
kutokana na sasa kuamua kutumia rasilimali za ndani katika kuinua
uchumi wa nchi hizo.
Kama alivyosema Rais Kikwete, jambo
muhimu na ambalo linapaswa kupewa kipaumbele kikubwa katika mikakati ya
kukuza uchumi wa Bara la Afrika, ni kuhakikisha kuwa Sera zinazoundwa
kusimamia uchumi zinakuwa bora na sahihi lakini pia kunakuwa na
ushirikiano mkubwa baina ya sekta ya umma na binafsi.
Tunafahamu kwamba si nchi zote za Afrika
zinakabiliwa na umasikini kutokana na kukosekana kwa uwezo wa
rasilimali watu au rasilimali fedha, kwani zipo zenye uwezo huo lakini
zinashindwa kufanikiwa kutokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa
viongozi katika kuongoza mapinduzi ya kiuchumi.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Serikali
ya Marekani kuanzia mwaka 2000 ilianza kutoa zawadi kwa nchi masikini
zinazoonesha jitihada za kujikomboa kiuchumi kwa kuzipatia miradi ya
Millennium Challenge Account (MCA) kwa lengo la kuziunga mkono ili
ziongeze juhudi na kasi zaidi lakini pia kuzifanya nyingine kuiga.
Kwa nchi kama Tanzania mafanikio ya
ukuaji wa uchumi yamejidhihirisha na ndio maana ilikuwa moja ya nchi
zilizonufaika na miradi ya MCC ambayo ukomo wake ni mwakani, lakini
ikiwa tayari imeahidiwa kupewa awamu ya pili ya miradi hiyo kutokana na
namna ilivyosimamia utekelezaji bora wa miradi hiyo ya maendeleo na ile
ya kijamii.
Chapisha Maoni