HOME
Nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania, ina mifumo ya shule inayotoa elimu bandia na hatimaye wasomi bandia.
Hii ni kinyume na hali iliyokuwapo miaka ya mwanzo ya uhuru. Kipindi hicho tulikuwa na elimu halisi iliyoegemea katika sera ya ujamaa na kujitegemea. Leo ni wapi tulipojikwaa?
Wasomi wa vyeti wataiendeleza nchi yetu?
Hii ni kinyume na hali iliyokuwapo miaka ya mwanzo ya uhuru. Kipindi hicho tulikuwa na elimu halisi iliyoegemea katika sera ya ujamaa na kujitegemea. Leo ni wapi tulipojikwaa?
Hivi sasa tuna wasomi wengi hata wa shahada za
uzamivu (PhD) wanatambulika kwa vyeti tu, huku wakikosa maarifa na
ubunifu katika utendaji kazi wao.
Hayo ni matunda ya elimu bandia. Wengine
wanatafuta vyeti usiku na mchana, wananunua alama vyuoni, ili tu wapate
shahada hata kama kichwani hakuna kitu!
Dhima kuu ya elimu na mchakato wa kujifunza ni
kumpa binadamu nguvu za kuweza kuikabili dunia, nguvu za kutafuta majibu
ya matatizo na changamoto zinazomsonga.
Pia kumpa nguvu za kuitawala dunia kwa kubuni nyenzo za kumwezesha kuishi maisha ya furaha. Hiyo ndiyo elimu tunayoipigania.
Kama kusudio kuu la elimu yetu ni kupata nyenzo za
kuitawala dunia na kunufaika nayo, ni wazi kwamba elimu ya kweli ni
lazima ikuze vipaji vya watoto wetu na mifumo ya utoaji vipaji
iendelezwe kwenye mazingira halisi ya dunia.
Sehemu kubwa ya kukuza vipaji na vipawa vya watoto
ni nje ya darasa. Huko ndiko iliko dunia ambayo wakihitimu masomo yao
wanaikuta na kuikabili.
Vyumba vya madarasa vinachangia kwa kiasi kidogo ukuzaji wa umahiri na talanta zinazojenga nguvu ya kuitawala dunia.
Maana dunia haiko ndani ya darasa, ni mazingira yote yanayotuzunguka pamoja na mwingiliano wa watu katika shughuli za kila siku.
Ndiyo maana, mitalaa ya elimu kwa kipindi cha
nyuma ilikazia elimu nje ya darasa kwa kusisitiza zaidi mitalaa ziada
(extra curricula) na mafunzo kwa vitendo yaliyokuwa yanawapa ujuzi wa
moja kwa moja watoto wetu.
Hata walioshindwa masomo darasani au kukosa nafasi
za kuendelea na elimu ya juu, waliweza kuishi maisha mazuri kwa kufanya
kazi za mikono zilizowaingizia kipato cha kutosheleza mahitaji yao na
hata ziada. Hawa waliandaliwa kuzikabili changamoto za dunia.
Nakumbuka tulikuwa tukifika shule, tunakimbia mchakamchaka umbali mrefu asubuhi kabla kuanza usafi au kuingia darasani.
Tulikuwa tukifagia maeneo ya shule na kupanda miti
na kumwagilia iliyokuwa inazunguka shule ili kulinda mazingira na
kukuza uelewa wa umuhimu wa kutunza mazingira.
Tuliingia darasani kwa saa kadhaa na ndani ya saa
hizo, tulitolewa nje mara nyingi ili tujifunze dhana mbalimbali ambazo
zilikuwa ni mifano halisi ya mafunzo yetu.
Tulikuwa na miradi ya shule kama bustani, elimu ya
ufundi kama kushona kufuma, kuchonga na hata ufugaji wa kuku na mbuzi.
Haya yote yalimwandaa mwanafunzi kuiishi dunia ya kesho, ili akimaliza
shule awe na nguvu za kupambana na maisha.
Mwanafunzi aliyelima hawezi kushindwa kujitafutia
chakula akimaliza shule. Mwanafunzi aliyekimbia mchaka mchaka hawezi
kushindwa kukimbia akimaliza shule, mwanafunzi aliyepanda miti akiwa
shuleni, hawezi kushindwa kupanda miti akimaliza shule.
Mwanafunzi aliyefundishwa ufundi akiwa shule,
hawezi kushindwa kujitegemea na kujitengenezea kipato akimaliza shule.
Mwanafunzi aliyechanganya kemikali akiwa shule, hawezi kushindwa
kuchanganya akihitimu masomo yake.
Aliyefua nguo akiwa shule, hawezi kushindwa kufua
nguo zake akimaliza shule, aliyefundishwa kufuga mbuzi akiwa shule,
hawezi kushindwa kufuga mbuzi akimaliza shule.
Aliyefundishwa kuitafiti dunia akiwa shule, hawezi
kushindwa kuitafiti dunia akimaliza shule. Mwanafunzi aliyefundishwa
kujitegemea akiwa shule, hawezi kushindwa kujitegemea akimaliza shule.
Mtu aliyeelimika ni lazima awe na nguvu ya kubuni
fursa za kuikabili dunia. Mabadiliko ya maendeleo yake kiakili na
kijamii ni lazima yaonekane bayana.
Hata hivyo, hali ya sasa nchini ni ya kusikitisha.
Mifumo ya shule inawataka watoto wetu wafungiwe darasani na wakariri
anachoandika mwalimu ubaoni tu.
Baada ya hapo wanatungiwa mtihani na kurudishwa
kwenye jamii kwenda kupambana na mitihani ya maisha huku wakiwa hawana
nguvu za kupambana.
Ndiyo maana tunaona hata mwanafunzi aliyehitimu
shahada ya uzamili, analalama kutafuta kazi ya kuajiriwa. Hana mbinu za
kuikabili dunia, maana alifundishwa kukariri tu dhana za wanafalsafa
waliokufa siku nyingi ambazo nyingi hazina uhalisia ndani ya utandawazi.
Hakupewa ubunifu na ujasiri wa kuikabili dunia, bali alipewa
nguvu ya kufaulu mitihani tu. Mwalimu Nyerere aliona mbali. Katika
utawala wake alisisitiza wanafunzi kuitawala dunia kwa kufanya karibu
kila kitu wakati bado wako shuleni.
Walitumia muda mchache kuwa darasani, muda mwingi
walikuwa nje ya darasa wakibuni, wakitafiti, wakijifunza kufanikiwa kwa
kuijua dunia. Ndiyo maana wanafunzi walimaliza shule wakiwa na afya
njema, wenye maarifa na mbinu nyingi za kuyakabili maisha.
Kwa sasa kinachosisitizwa ni kujenga madarasa ili
wanafunzi wafungiwe humo wakati wote. Hakuna kutoka nje kujifunza
uhalisia wa dunia.
Hakuna kwenda ziara za mafunzo kukazia maarifa,
hakuna kazi za mikono na za akili zinazokuza uelewa, hakuna kwenda
maabara kuchanganya kemikali ili kuvumbua kitu.
Chapisha Maoni