HOME
SAKATA LA IPTL: Mabalozi waitaka Serikali kuchukua hatua kali
Dar es Salaam. Licha ya Rais
Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi wa sakata la uchotaji fedha kutoka
Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu na kutangaza kuchukua hatua
dhidi ya baadhi ya viongozi na watendaji, nchi wahisani wamesema bado
suala hilo linawachanganya na wanasubiri tamko la Serikali.
Nchi hizo, ambazo zilizuia takriban Sh1 trilioni
za ufadhili na kuchangia nakisi ya bajeti ya Serikali, juzi zilikiri
kuanza kuruhusu sehemu ya fedha hizo baada ya baadhi ya maazimio ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na
kumvua uwaziri Anna Tibaijuka, kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na kumuweka kiporo waziri wake,
Sospeter Muhongo na kusababisha Jaji Fredrick Werema kujivua wadhifa
wake wa Mwanasheria Mkuu.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshaeleza kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili juzi,
Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Timothy Clarke alisema kwamba
Serikali imeonyesha jitihada za mwanzo, lakini wanasubiri kuona hatua
kali zaidi zikichukuliwa pamoja na kuja na kauli moja kuhusu fedha hizo.
Alisema alichobaini ni kwamba wananchi wengi
wanataka kujua hatima ya sakata hilo ndiyo maana walitumia vyombo vya
habari kufanya mijadala mbalimbali kuzungumzia wizi wa fedha za escrow
ambazo haijawekwa wazi kuwa ni za umma ama ni za Kampuni ya Kufua Umeme
ya IPTL.
Balozi Clarke alisema kwa upande mwingine,
Serikali imeonyesha tabia ya kusita katika kutoa uamuzi kwenye suala
hilo na kwamba walitarajia kusikia tamko kali pamoja na tamko la kuzuia
vitendo hivyo visiendelee.
Alieleza kuwa hadi sasa nchi nyingi hazijaipa
fedha Tanzania kama zilivyokuwa zinatarajiwa kwa kuwa bado zinasubiri
hatua zaidi kutoka serikalini.
Sakata la escrow, lililohusu uchotwaji wa Sh306
bilioni kutoka akaunti hiyo, lilisababisha Taasisi ya Marekani ya MCC
inayosaidia nchi zinazoendelea, kutangaza kusitisha kusaini mkataba wa
awamu ya mpango huo wa maendeleo kuishinikiza Serikali kushughulikia
kashfa hiyo.
Bodi ya Wakurugenzi ya MCC ilitoa taarifa yake
Desemba 16 mwaka jana, ikieleza kuwa mkutano wake wa Desemba 10 mwaka
huu uliruhusu kuanza maandalizi ya kusaini mkataba wa awamu ya pili ya
mpango huo, lakini ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa
inavyoendelea Tanzania.
Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia
mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na
Sh765 bilioni.
“Japokuwa bodi ilipiga kura kwa dhati kabisa ya
kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili,
inaihimiza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za
kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi
wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.
Sakata la escrow lilihusisha fedha zilizokuwa
zimehifadhiwa Benki Kuu wakati kesi baina ya Shirika la Umeme (Tanesco)
na IPTL zikipambana mahakamani. Pande hizo mbili zilikubaliana kufungua
akaunti hiyo ya escrow ili kutunza fedha ambazo Tanesco ilitakiwa iilipe
IPTL ikiwa ni malipo ya ununuzi umeme.
Hata hivyo, akaunti hiyo ilifungwa kwa njia ambayo ilitia shaka
na fedha hizo kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solution Limited
(PAP) ambayo ni mmiliki mpya wa IPTL na kukiwa na mambo mengi
yaliyotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya malipo hayo, ikiwa ni pamoja na
kulipwa kwa kodi ya Serikali na kukokotoa upya gharama ambazo Tanesco
ilitakiwa ilipe baada ya mzozo wao kuisha mahakamani.
Pia, fedha hizo zililipwa kwa James Rugemarila
aliyekuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL na ambaye baada ya
malipo alitoa mgawo wa fedha kwa watu kadhaa, wakiwamo viongozi wa dini,
watumishi wa umma, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa zamani, hali
iliyotia shaka zaidi kuhusu fedha hizo.
Tayari Tibaijuka amewajibishwa baada ya kupokea
Sh1.6 bilioni kutoka kwa Rugemarila, hali kadhalika Andrew Chenge,
ambaye pia alipewa Sh1.6 bilioni na William Ngeleja (40.4 milioni)
wametakiwa kuondolewa kwenye uenyekiti wa Kamati za Bunge sambamba na
Victor Mwambalaswa na Fredrick Werema, akitangaza kujiuzulu wadhifa wake
wa Mwanasheria Mkuu kwa maelezo kuwa ushauri wake haukueleweka na kuzua
tafrani.
Naye Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose
alisema mazungumzo na Serikali bado yanaendelea na kwamba hali
itaendelea kuwa nzuri kadri mazungumzo yanavyoendelea.
“Bado tunaendelea na mazungumzo na Serikali huku tukisubiri tamko,” alisema Dianna.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa mfuko wa
maendeleo wa wahisani, Sinikka Antila juzi ilieleza kuwa mpaka sasa
zimekwishatolewa Dola 84 milioni sawa na asilimia 15 ya msaada wote
kwenye bajeti ya 2014/2015.
Kwa upande wake, kiongozi wa mabalozi waliopo
nchini, Juma Mpango alisema Tanzania imeonyesha jitihada katika kuleta
maendeleo na kupambana na rushwa.
Balozi Mpango, ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema Serikali imeonyesha nia ya
kupunguza matukio ya kifisadi.
“Tumefuatilia namna ambavyo Tanzania imefanya vita
kubwa kuondoa madhara ya ufisadi katika nchi, ilikuwa kubwa sana,”
alisema Balozi Mpango.
Nchi na wadau wanaochangia kwenye bajeti na sekta
nyingine za maendeleo ni; Canada, Denmark, Finland, Ujerumani, Ireland,
Japan, Sweden, Uingereza, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuiya
ya Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB).
Chapisha Maoni