HOME
Siasa uchwara ni hatari kwa nchi'
WASOMI, wanadiplomasia na viongozi wa
dini wameasa wanasiasa kuwa makini na usalama wa taifa kwa kuhakikisha
tofauti za vyama vyao, hazidhoofishi utaifa na maslahi ya nchi.
Wamehadharisha juu ya kile kilichoitwa ‘siasa uchwara’ na propaganda,
wakisema ikifika hatua ya wanasiasa kuonesha tofauti hadharani juu ya
masuala yanayogusa maslahi na usalama wa nchi, ni jambo la hatari na
haileti picha nzuri usoni mwa mataifa mengine.
Hoja hizo zimetolewa na watu hao wa kada
tofauti wakati wakizungumzia yaliyojiri bungeni juzi wakati Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipowasilisha
bajeti yake iliyopitiwa.
Kambi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa
Msemaji wa wizara hiyo, Ezekiah Wenje, katika sehemu kubwa ya hotuba
yake, alijenga hoja za kuisemea Rwanda huku akishutumu Waziri Membe
kwamba ni chanzo cha kudorora kwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda.
“Naogopa sana tunapoanza kuonesha
tofauti zetu hadharani, malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wa nchi yetu
ni vyema tusiyazungumze bungeni na mahali pengine popote,” alisema
Mwanadiplomasia, Balozi Charles Sanga.
Alisema anaamini watanzania wote
wanapenda nchi yao. Alishauri, “Tukiri tujisahihishe, naamini ulimi
uliteleza, hivyo tukiri kukosea na tujisahihishe, wajibu wa kutunza na
kulinda tunu zetu,(amani, uzalendo, utu) zinalindwa na kuheshimiwa”.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema siyo jambo la busara wanasiasa
kuchochea ugomvi na nchi jirani. Bashiru alisema kufanya hivyo ni
kuhatarisha usalama uliopo ndani ya nchi na hata barani Afrika, hivyo
kuwa kichocheo cha ukoloni mamboleo.
Alisema ni vyema wanasiasa, wakaacha
mara moja siasa uchwara zinazochochea Utaifa finyu, aliosema unalenga
kutekelezwa kwa maslahi ya vikundi vya propaganda na vyama vyenye
maslahi binafsi.
“Tuangalie siasa za utaifa kwanza,
kuliko vyama vyetu na maslahi binafsi, vikundi vya propaganda hapa siyo
eneo lake, huwezi kuchezea utaifa, ni kuhatarisha usalama,” alionya
Bashiru.
Kuhusu maslahi ya taifa, mhadhiri huyo
ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Sayansi ya Jamii, alisema zipo aina
mbili za kusimamia jambo hilo.
Alitaja kwamba moja ni nchi yenyewe kwa
sera na viongozi wake; na pili ni ushirikiano wa wananchi ndani ya nchi
husika. Alisema jambo hilo, lilipaswa kufanywa hivyo na siyo kugawanyika
bungeni kwenye masuala ya maslahi ya taifa.
“Nataka hawa wanasiasa wajue kwamba hivi
sasa vitisho vya usalama vina sura mpya, ikiwemo ya ukoloni, sasa
tunapoanza kujigawa wakoloni wanapata nguvu na mfahamu kuwa yapo mataifa
yanayopenda kuona mkilumbana na wanaweza kuwasaidia ili mgombane
vizuri, iwe rahisi wao kuja,” alisisitiza Bashiru.
Alisema ni vyema wananchi na wanasiasa
wasiofahamu, wakajua kuwa Tanzania kupeleka majeshi yake Kongo haikuwa
bahati mbaya wala makosa, bali ni jambo jema kwani nchi imekuwa mstari
wa mbele tangu zamani kutetea na kuhakikisha ukombozi wa nchi jirani na
Afrika kwa ujumla, wanapata uhuru.
“Majeshi yetu yanapokwenda nje ya mipaka
ya nchi, siyo jambo baya, ni jema kwa maana Afrika ni moja na ulinzi wa
bara hili, unapaswa kufanywa na waafrika na siyo wazungu, tukiwaacha
hao wazungu waje kutulinda, nia yao siyo kulinda bali pia kupora
rasilimali zetu, walifanya hivyo Kongo”, alifafanua Bashiru.
Aliongeza, sasa nchi ina taswira nzuri
ndani na nje ya Afrika, hasa kwa kusaidia ukombozi na usuluhishi wa
migogoro na pia kuifanya Afrika kuwa moja, hivyo kuanza kuchokoana
wenyewe ni kudhoofisha usalama.
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo
la Bukoba, Method Kilaini alisema siyo vyema Watanzania kuanza
kulumbana juu ya utetezi wa maslahi ya nchi.
Alisema Wenje alipaswa kufahamu kwamba
watanzania wote, wana wajibu wa kutetea nchi yao popote hasa linalokuja
suala la maslahi ya taifa.
“Tusiongeze machungu yaliyopita, suala
la M23, sio tatizo tena, lilishakwisha, jambo la msingi hapa ni kutafuta
uhusiano mzuri na jirani zetu, tuyamalize, tukae vizuri na siyo
kuchochea ugomvi, tukumbuke tuko nao jirani na tunashirikiana kwa njia
moja au nyingine, wanasiasa wasiongeze ugomvi", alisisitiza Askofu
Kilaini.
Mwingine aliyezungumzia ni Shehe wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Alhad Mussa alishangaa Watanzania wanaotanguliza
maslahi ya nchi nyingine, badala ya nchi yao na kusema ni jambo la
kushangaza.
“Tuwe wazalendo na nchi yetu, tuwaambie
ukweli watanzania, tusiwapotoshe, tuna wizara husika ya kuzungumza mambo
ya uhusiano na mataifa mengine, tuiheshimu, tuiamini, ni chombo chenye
mamlaka kamili,” alisisitiza Mussa.
Katika kujibu hoja za Wenje alizotoa
bungeni, Waziri Membe katika kuhitimisha mjadala, alieleza kushangazwa
na kitendo cha mbunge huyo, kuisemea nchi nyingine bungeni.
Waziri Membe alisema huo ni uchonganishi
na unaweza kuifikisha nchi pabaya. Alitaka wabunge na viongozi wengine,
kuwa wazalendo na kutetea maslahi ya taifa kwanza.
Chapisha Maoni